6/recent/ticker-posts

Sangoma apigwa stop kutoa huduma Z’bar

Na Fatma Kassim
BARAZA la Tiba Asili na Tiba Mbadala Zanzibar, limemfungia mganga wa kienyeji kutoka Rufiji, Omar Ali, kufanya shughuli zake za kiuganga Zanzibar kutokana na kukosa sifa za kufanya kazi hiyo.

Mrajis wa Baraza hilo, Haji Juma Kundi, alisema  uamuzi huo umekuja kutokana na kuwepo wimbi kubwa la waganga wasio na uwezo wa kufanya tiba hiyo na badala yake wanawadanganya wananchi.

Alisema mganga huyo kwa kushirikiana na wenziwe  wanazunguka  katika vijiji tofauti na wanatumia njia mbali mbali za kuwadanganya watu kuwa wamefanyiwa ubaya ili kujipatia fedha kwa urahisi.

Alisema kufanya hivyo ni kinyume na utaratibu wa baraza hilo ambapo wanafanya shughuli hizo bila ya kuwa na vibali vinavyotolewa na baraza hilo.

Aliwataka wananchi wote wenye nia ya kufanya shughuli hizo wafike katika baraza hilo kufuata maelekezo ambayo  yatawezesha waganga hao kufanya kazi zao kwa utaalamu.


Kwa upande wa mganga huyo, alikiri kuwa yupo katika shehia mbali mbali kwa nia ya kuwapatia tiba wananchi wenye matatizo kwa kutumia vielelezo alivyotoka navyo Tanzania Bara ambavyo havitambuliwi Zanzibar.

Aliomba kuongezewa muda wa kufanya shuguli zake kutokana na kuwa ameshawaanzia dawa watu wengi.

Wakati huo huo baraza hilo limefanya zoezi la kuwakamata wauza dawa za asili katika sehemu za misikiti na sehemu zilizowazi kutokana na kuwa dawa wanazouza kukosa ubora na kusababisha maradhi mbali mbali kwa watumiaji.


Mrajis wa Baraza hilo alisema wameamua kufanya zoezi hilo kutokana na kuwa hivi sasa kumekuwa na wimbi kubwa la wauza dawa katika sehemu za misikiti na sehemu za wazi ambazo zinakuwa si salama.

Post a Comment

0 Comments