6/recent/ticker-posts

Tanzania yasaini makubaliano kutokomeza udhalilishaji

Na Mwandishi wetu
TANZANIA imetia saini rasmi hati ya makubaliano ya mkutano wa mtoto wa kike uliofanyika mwaka jana nchini Uingereza.
Kwa mujibu wa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto wa Tanzania, Sophia Simba, kusaini kwa hati hiyo, ni kuonyesha dhamira ya serikali ya nchi hiyo katika kupambana na kuhakikisha inatokomeza vitendo vya ukeketaji na ndoa za utotoni.
Utiaji saini huo, umefanyika mbele ya wawakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu, UNFPA, Balozi wa Uingereza nchini Tanzania na wawakilishi kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali.
Takwimu nchini Tanzania zinaonesha  katika kila watoto watano wa kike, wawili kati yao wanakeketwa huku wengine wakipitia ndoa za utotoni hali inayowanyima watoto wa kike haki zao za msingi ikiwemo kupata elimu.
"Kimsingi ukeketaji na ndoa za utotoni zinawakwaza watoto kimasomo na kukosa afya njema na kuathiri maendeleo ya Tanzania. Nchi zinazoruhusu watoto wote wa kike kwenda skuli na kukamilisha elimu yao, hizi ndizo ambazo zina mafanikio makubwa katika kupunguza umaskini," alisema Dianna Melrose, Balozi wa Uingereza nchini Tanzania.
Baadhi ya wanaharakati, akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Valerie Msoka walisema kutofanikiwa kwa mapambano hayo mara nyingi kunasababishwa na kukosekana utashi wa kisiasa.
Mkoa wa Shinyanga ndio unaoongoza nchini Tanzania kwa mimba na ndoa za utotoni.
Takwimu kutoka mashirika mbalimbali ikiwemo UNICEF zinaonesha kwa siku, watoto 16 wanapewa mimba za utotoni.

Kwa mujibu wa wataalamu, hali hiyo imekuwa ikiendelea kwa muda mrefu na kwa asilimia kubwa imezorotesha maendeleo ya mtoto wa kike.

Post a Comment

0 Comments