6/recent/ticker-posts

Balozi Seif awataka vijana kisiwani Pemba kubadilika

  Baadhi ya Vijana wa Chama cha Mapinduzi wa Jimbo la Chake chake Pemba  wakifuatilia hotuba na Mke wa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mama Asha Suleiman hayupo pichani wakati akizungumza nao kwenye ukumbi wa Hoteli ya Hifadhi Chake chake Pemba.
 Mke wa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mama Asha Suleiman akibadilishana mawazo na Vijana wa CCM Jimbo la Chake chake katika Kikao cha kutafakari zoezi zima la Kampeni na kuelekea kwenye uchaguzi Mkuu.
  Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Vijana wa CCM Jimbo la Chake chake kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Hifadhi Chake chake Pemba.

 Balozi Seif Ali Iddi akipokea baadhi ya Kadi za Wanachama wa Chama cha Wananchi { CUF } walioamua kukihama Chama hicho na kujiunga na Chama cha Mapinduzi hapo Hifadhi Hoteli Chake chake Pemba.

Baadhi ya Vijana wa CCM wakifuatilia hotuba ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Taifa Balozi Seif hayupo pichani wakati akizungumza nao hapo Hifadhi Hoteli Chake chake Pemba.

Picha na – OMPR – ZNZ

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmshauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi amewanasihi Wananchi hasa Vijana wa Majimbo la Kisiwa cha Pemba kubadilika kwa lengo la kuachana na tabia ya kufanywa  ngazi na baadhi ya Watu wakati wa uchaguzi na baadae kuamua kujinufaisha wao binafsi na familia zao.

Alisema  miaka isiyopunguwa ishirini  wananchi hao  wamekuwa wakitumiwa kama vitega uchumi na watu ambao wamekuwa na hulka ya kuwakimbia mara tu baada ya kuwachagua.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa nasaha  hizo wakati akizungumza na Vijana wa Chama cha Mapinduzi wa Jimbo la Chake chake wakiwemo pia  wale Vijana walioamua kuacha chama cha Wananchi { CUF } na kujiunga na CCM Mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Hifadhi Tibirinzi Chake Chake Pemba.


Alisema Wananchi na hasa Wanachama wa vyama vya siasa wana haki ya kubadilisha sera kwa kuamua  kuhama   chama ambacho wanahisi sera zake hazitekelezeki wala kuwaletea maendeleo yao.

Balozi Seif ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya Uchaguzi ya CCM  Zanzibar alieleza kwamba watu wanaoufanya Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na Ubunge wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ni ajira waelewe kwamba wanawaumiza Wananchi walioamua kuwachagua.

Alifahamisha kwamba kazi za Wabunge na Wawakilishi ni kuwatumikia Wananchi na ile tabia ya baadhi yao kutumia mafungu ya fedha za mafao yao kuanza kuhonga  wananchi wakati unapokaribia uchaguzi ili wachaguliwe tena wafahamu kwamba wanafanya dhambi ambayo siku moja itawahukumu.
Aliwapongeza Vijana walioamua kuachana na vyama vya upinzani na kujiunga na Chama cha Mapinduzi chenye kujali  na kuheshimu watu wenye dini, kabila na rangi tofauti.

Mapema Mke wa Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Mama Asha Suleiman Iddi  alisema mchezo unaochezwa na Wananchi hasa Vijana wa Majimbo ya Pemba  wa kuwakubalia Viongozi wasiotimiza wajibu wao utaendelea kuwaathiri wenyewe.

Mama Asha alisema Viongozi hao wanachofanya baada ya kuchaguliwa na Wananchi ni kuelekeza nguvu zao katika kuimarisha maisha yao pamoja na kuwajengea hatma njema watoto wao binafsi kielimu.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Vijana hao Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi Tanzania { UVCCM } Shaka Hamdu Shaka alisema mabadiliko ya uongozi Pemba yanaweza kupatikana endapo Wananchi wenyewe wataamua kuyasimamia ipasavyo.

Shaka alisema mazingira ya ushindi wa CCM katika uchaguzi Mkuu unaokaribia katika nafasi zote  za Uongozi Kuanzia Udiwani Hadi Rais ndani ya Kisiwa cha Unguja uko wazi na kinachosubiriwa kwa hivi sasa ni Tarehe ya kuapishwa kwa washindi hao.


Post a Comment

0 Comments