6/recent/ticker-posts

Chagueni viongozi wa CCM watawaletea maendeleo - Wito


  
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Pemba                                  11.10.2015
---
WANACCM na wananchi kisiwani Pemba wametakiwa kutowachagua viongozi wa vyama vya upinzani kikiwemo chama cha CUF kwani wamekuwa wakiwafanya vitega uchumi na badala yake wawachague viongozi wa CCM ambao watawatekelezea mahitaji yao na kuwaletea maendeleo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano wa Kampeni ya uchaguzi wa CCM uliofanyika uwanja wa Pujini, Jimbo la Chonga, Wilaya ya ChakeChake, Mkoa wa Kusini Pemba, viongozi wa CCM waliohudhuria mkutano huo walisema kuna kila sababu ya kuwachagua viongozi wa CCM ambao watakuwa nao wakati wote wa shida na raha.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM ambaye pia, ni Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi aliwataka wananchi wa Pemba kufanya mabadiliko na kuwaeleza kuwa viongozi wa CUF wataendelea kuwafanya vitenga uchumi kama hawakuwatambua ujanja wao kuwa wakishakuwachagua tu huwakimbia.

Alisema kuwa viongozi wa chama cha CUF hawana nia ya kuwapa maendeleo, na kueleza kuwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kuna Mifuko ya Majimbo ambapo viongozi hao hupewa fedha kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wao Majimboni.


Balozi Seif alitolea mifano ya Majimbo ambayo hayafaidiki na mifuko hiyo kama likiwemo Jimbo la Mji Mkongwe ambalo Mwakilishi ameukacha Mfuko huo na kuwanyima wananchi waliomchagua kuwanyima fursa ya kuatekeleza miradi ya maendeleo ambayo wangeliitekeleza kupitia mfuko huo.

Alisema kuwa iwapo watawachagua viongozi wa CCM watakuwa karibu nao na watafaidika na Mfuko huo pamoja na kuwasaidia katika kutekeleza miradi ya mbali mbali ya maendeleo Majimboni mwao.

Balozi Seif aliwasisitiza kutokubali kuuza vitambulisho vyao vya kupigia kura pamoja na kuwatahadharisha wanaCCM kwa wale vijana wa CUF wanaochukua sare za CCM kuwa waangalifu nao ili wasije kuzitumia kwa lengo la kuwahujumu wanaCCM.

"Watu hawa hawana nia njema kwani wamekuwa wakisema kuwa mara hii CCM watatukoma...najua maana ya neno hili ni kufanya vurugu lakini wajue kuwa vyombo vya ulinzi vipo",alisema Balozi Seif.

Aidha, Balozi Seif Alisema kuwa viongozi wa CUF wamekuwa wakiwadanganya wananchi na wafuasi wao kuwa mwaka huu watashinda uchaguzi jambo ambalo haliwezekani na kusisitiza kuwa mwaka huu ndio mwisho wa chama cha CUF.

Aliwataka wanaCCM kuendelea kupamba bendera zao na picha za viongozi wao pamoja na kupamba Maskani, nyumba na Matawi yao kwa lengo la kusherehekea ushindi wa CCM kwani ndio chama kinacholeta maendeleo Zanzibar.

Alisisitiza kuwa chama cha  CUF hakina lengo la kuwaletea maendeleo wananchi wao na kazi yao baada ya kupata uongozi ni kuwakimbia wananchi waliowachagua na kwenda katika miji ya Dodoma, Unguja na Dar-es- Salam.

Waziri wa Maji, Ardhi na Nishati ambaye pia, ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Ramadhan Abdalla Shaaban aliwataka wananchi wa kisiwa cha Pemba wasikubali kudanganyika kwa suala la mafuta kama linavyozungumzwa na vyama vya upinzani.

Alisema kuwa suala la mafuta na gesi litachukua muda mrefu sana kutekelezwa na kueleza jinsi juhudi zilivyochukuliwa na Dk. Shein katika kulisimamia suala hilo na kuliendeleza vyema kwa mashirikiano na Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Alisema kuwa CCM inatenda na itaendelea kutenda yale yote inayoyaahidi na kuwataka wananchi wa Pemba kuwachagua viongozi wa CCM ili kwenda vizuri na kupata maendeleo.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Maua Abeid Daftari kwa upande wake alisema kuwa Dk. Shein ametekeleza vyema  Ilani ya Uchaguzi ya CCM hivyo kuna haja ya kumchagua ili aendelee kuwa Rais wa Zanzibar.

Alisema kuwa Dk. Magufuli na Dk. Shein ni wachapa kazi na amefanya nao kazi na anawafahamu vizuri huku akisisitiza kuwa wanaweza kuongoza kutokana na uzoefu mkubwa na uadilifu wao.

Aliwataka wananchi wa Wilaya ya Chake likiwemo Jimbo la Chonga hasa Pujini kuwachagua viongozi wa CCM ili wawasaidie katika kuwaletea maendeleo kwani hao waliowachagua katika uchaguzi uliopita hawawasaidii wananchi wao na wamekuwa wakichukua fedha kwenye vyombo vya kutunga sheria na kufanyia shughuli zao binafsi.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Asha Abdalla Juma alieleza sababu mbali mbali za kuwachagua viongozi wa CCM kwani wana sifa za kutosha, waadilivu, makini, wakweli na wachapakazi na kuwataka wawachague.

Akizieleza sifa za Mama Samia Suluhu Hassan, Asha alisema kuwa wanawake wanaweza na wataendelea kuweza ndani ya CCM na kukipongeza chama hicho kwa kuwajali wanawake na hatimae kuwapa uongozi mkubwa.

Alisema kuwa Mama Shein na Mama Balozi wametoa milioni 389 kwa vikundi mbali mbali vya akina mama Unguja na Pemba ambapo miongoni mwa fedha hizo milioni 54 vilipewa vikundi vya Pemba na kusema kuwa hiyo yote ni azma yao ya kuwasaidia wanawake kupata maendeleo.

Asha alieleza kuwa uchumi wa Zanzibar umeimarika chini ya uongozi wa Dk. Shein, na kumsifu hatua alizochukua katika kusimia maendeleo ya nchi sambamba na kuongezeka kwa uajibikaji kwa wafanyakazi.

Aliwataka wananchi kumchagua Dk. Magufuli kwa lengo la kuendeleza na kuimarisha Muungano, Samia Suluhu pamoja na Wabunge, Wawakilishi, Madiwani.

Kaimu Katibu Mkuu wa Vijana Tanzania Shaka Hamdu ambaye pia, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM alisema kuwa ASP ya mzee Karume ndio CCM ya leo kutokana na kutekeleza vyema ahadi zake na kuwaomba vijana wenzake kuendelea kuiunga mkono CCM.

Aliwahakikishia wananchi wa Pemba kuwa ushindi wa CCM hauepukiki na Dk. Shein ndio atakae kuwa Rais kwani ni muungwana na bingwa kwa kuahidi na kutekeleza ambaye pia, ni mvumilivu na MwanaCCM kindakindaki.

Aliongeza kuwa Dk. Shein ni jasiri wa kusimamia maendeleo na kuwaambia kwua kupiga kura ndio haki ya msingi lakini kumwaga damu haikubaliki Tanzania hivyo wasidanganyike na wale wasio hubiri amani na utulivu .

Shaka alisisitiza amani na utulivu na kuwaasa vijana kuimarisha umoja wao na kueleza kuwa kwa wale wote wanaotumia majukwa kutangaza kuvuruga amani hawana maslahi na wananchi.

Aliwataka wanaCCM na Wananchi mara baada ya kumaliza kupiga kura warudi majumbani na kusema kuwa CCM ni chama kikubwa na kueleza kuwa kusimamishwa kwa Dk. Shein kuwa mgombea urais wa Zanzibar haikubahatishwa.

Alisema kuwa CCM ilitambua kuwa mgombea nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia UKAWA hana soko na atakapokatwa kwenye CCM anakwenda upinzani na huko anakwenda kuvimaliza vyama vya upinzani.

Alitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa kuandaa mazingira mazuri ya ajira kwa vijana.

Nae Modelin Kastiko alieleza mafanikio yaliopatikana katika sekta ya elimu na maji pia, alieleza kuwa hapo siku za nyuma kulikuwa na matatizo makubwa ya maji ambapo kwa hivi sasa tatizo hilo limebaki kuwa historia.

Nao viongozi wa Mkoa wa Kaskazini kwa nyakati tofauti walisisitiza haja ya kuendelea kusimamia amani na utulivu na kuwataka vijana wanaotumiwa kuja kufanya fujo siku ya uchaguzi kuachana na azma yao hiyo.

Viongozi hao walieleza kuwa WanaCCM wa Wilaya ya ChakeChake waliahidi kuwa kura zote watapewa wagombea wa CCM, huku wakimuhakikishia ushindi Dk. Shein kuendelea kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

Post a Comment

1 Comments

  1. Inamaana hawa CCM hadi leo wanafikiri vijana wapo na mawazo yale yale ya 1964? miaka zaidi ya 50 hatukuwahi kuona wabunge wa CCM wakituletea hizo pesa wanazopewa bungeni seuze leo!!! safari hii vijana tumeamua ni mabadiliko kwenda mbele ccm inafaa kukaa chonjo kusubiri 1920 kuja na sera nyingine.

    ReplyDelete