6/recent/ticker-posts

Dk Shein Awahutubia Wananchi wa Pujini Amewataka Kuimarisha Lugha ya Kiswahili na Kuifanya Lahaja za Kiswahili Zanzibar.

Na Mwandishi Wetu Pemba.
MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. Ali Mohammed Shein amesema kuwa juhudi za kuimarisha lugha ya Kiswahili na kuzifanya lahaja za Kiswahili za Zanzibar kuwa chimbuko la Kiswahili fasaha zitaendelezwa katika miaka mitano ijayo chini ya uongozi wa chama hicho.

Akizungumza na wananchi pamoja na WanaCCM waliohudhuria katika mkutano wa Kampeni za uchaguzi kwa upande wa CCM uliofanyika uwanja wa Pujini, Jimbo la Chonga, Wilaya ya ChakeChake, Mkoa wa Kusini Pemba, Dk. Shein alisema kuwa tayari Kamusi za lahaja za Kipemba, Kimakunduchi na Kitumbatu zimechapishwa na kusambazwa kwa wananchi.

Alisema kuwa hatua ya ukaguzi wa kazi za sanaa kwa lengo la kulinda na kuhifadhi mila, desturi na silka za Mzanzibari imetekelezwa na kusisitiza kuwa kituo kikuu cha lugha ya Kiswahili kwa nchi za Afrika Mashariki kitakuwa Zanzibar kwani ndio chimbuko ya lugha ya Kiswahili.

Akieleza kuhusu uimarishaji wa viwanja vya michezo, Dk. Shein alisema kuwa tayari uwanja wa Amani umewekewa nyasi za bandia, njia za kukimbilia na kwa upande wa uwanja wa mpira wa Gombani Pemba nao umeiwarishwa kwa kuwekewa nyasi za bandia, taa, kujengwa paa jipya na hivi sasa mchakato wa ujenzi wa  njia za kukimbilia unaendelea katika kiwanja hicho.


Aidha, Dk. Shein alisema kuwa ujenzi wa kiwanja kipya cha michezo cha Mao Tse Tung unatarajiwa kuanza mapema mwezi Februari mwaka ujao hatua ambayo baada ya kukamilika kwa ujenzi huo wa kiwanja kipya na cha kisasa kitasaidia kwa shughuli za michezo na sherehe za kimataifa.

Tayari Sera na Sheria zinazoongoza Utamaduni zimefanyiwa mapitio ili kukidhi matarajio na mahitaji ya wakati na sheria mpya ya Baraza la Sanaa na Sensa ya Filamu na Utamaduni imetungwa.

Ambapo chini ya Sheria hiyo Bodi ya Sensa ya Filamu na Baraza la Sanaa la Zanzibar vimeunganishwa.

Pamoja na hayo, utafiti wa Urithi wa Utamaduni usioshikika umefanyika na matokeo ya utafiti huo yameweza kuhifadhiwa Kimataifa na kuingizwa katika orodha ya UNESCO ya tamaduni zinazohifadhiwa.

Sambamba na hatua hiyo matokeo ya utafiti huo pia, yamerejeshwa kwa wananchi wa maeneo husika ili kuzitumia kama sehemu ya ajira na kupambana na umasikini.


 Dk. Shein alitumia fursa hiyo kusisitiza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Znzibar chini ya uongozi wa CCM kuimarisha sekta ya michezo nchini huku akisisitiza kupewa kipaumbele kwa michezo yote pamoja na wanamichezo wake. 

Post a Comment

0 Comments