STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 17.10.2015
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein ameendelea
kuwasisitiza wananchi na wanaCCM kuitumia vyema haki yao ya msingi ya kupiga
kura siku ya Oktoba 25 mwaka huu na kuwataka mara tu baada ya kumaliza upigaji
kura warudi majumbani.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo
kuwasisitiza wananchi na wanaCCM kuwa kwa mujibu wa Sheria za Tume ya Uchaguzi chombo
chenye mamlaka ya kulinda kura siku hiyo ni Tume hiyo ya Uchaguzi na kwa
kushirikiana na Vyombo vya dola vyote kwa pamoja vitahakikisha hilo linatendeka
na kuwataka wananchi hasa vijana kutokubali kutumiliwa na watu wachache katika
kuvuruga amani.
Hayo aliyasema leo katika uzinduzi wa
Tawi jipya la CCM la Mombasa Kwamchina, liliopo Wilaya ya Dimani, Mkoa wa
Magharibi Kichama, Jimbo la Kiembesamaki Zanzibar.
Aidha, DK. Shein ambaye pia, ni Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliwataka wananchi baada ya
kumaliza kupiga kura warudi majumbani na kusubiri kutangaziwa mshindi na kuwaeleza
kuwa ulinzi wa kisheria wa kura ni wa vyombo vya kisheria vilivyowekwa maalum.
Dk. Shein aliwahakikishia wanaCCM kuwa atarudi
Ikulu baada ya kura nyingi watakazompa wananchi kutokana na kumkubali na
kuzikubali Sera za chama chake.
Aidha, alitoa pongezi kwa Balozi Seif Idd
kwa kufanikisha kupatikana kwa kiwanja hicho
pamoja na wanaCCM wote waliowezesha ujenzi huo na kueleza kuwa jitihada zake na
zile za wanaCCM za kukilinda na kukitetea chama na juhudi za Serikali ndio sababu
za kuhemkwa kwa wapinzani.
Alisifu hatua za kujitolea ndani ya chama
cha CCM ambazo juhudi hizo zilianzwa na muwasisi wa ASP Mzee Abeid Karume na
kusema kuwa CCM ina kila sababu ya kufanya juhudi kutokana na historia yake
kwani ndio chama chenye historia ya ukombozi wa Zanzibar na kueleza kuwa kamwe vyama
vyengine haviwezi kulingana na CCM.
Alisema kuwa viongozi wa CCM ni viongozi
mahiri na wana uwezo wa kuongoza Dola na ndio Zanzibar imeweza kupata mafanikio
kutokana na uongozi wa CCM na kuwasisitiza wanaCCM kuendeleza wajibu wao,
wakitumikie chama na Serikali yao.
Alisema kuwa ujenzi wa jengo hilo unaenda
sambamba na mradi wa CCM wa kumarisha chama, na kutolea mfano wa kuzinduliwa
kwa jengo jipya la CCM huko Dodoma mwezi Julai mwaka huu, ujenzi wa jengo la
UVCCM lenye ghorofa 32 lililojengwa huko
Dar-es-Salaam yote hayo ni uamuzi thabiti wa kuiimarisha CCM.
Dk. Shein, alipongeza azma ya Tawi hilo ya
kujenga maduka, mafunzo ya kompyuta, ushoni na ukodishwaji wa ukumbi wa
mkutano,kuwaenzi wajasiriamali, shughuli za kijamii na kuwataka kuongeza kasi
katika mipango hiyo kwa lengo la kuimarisha maslahi ya wanaCCM wa Tawi hilo.
Aidha, Dk. Shein alifurahishwa na azma ya
Tawi hilo kutoa elimu ya itikadi na kutoa nasaha kwa vijana kutokuba kupotoshwa
na watu wasioitakia mema nchi yao ambao wako tayari kufanya lolote kwa ajili ya
kulinda maslahi yao binafsi, bila ya kujali hali na maisha ya wengine.
Dk. Shein aliwahimiza vijana kujitokeza
kwa wingi huku wakiwa na ari na hamasa ya kupokea mafunzo hayo ya itikadi na
historia ili wawe na moyo wa kizalendo na utayari wa kuitumikia na kuilinda
nchi yao.
Ni jukumu lao la kuwaeleza historia ya
chama chaio kilipotoka, kilipo na kinapokusudia kwenda na kama hakikufanyika
hicho ndipo vijana wanapoanza vurugu barabarani.
Kuna kila sababu ya kuwafundisha vijana
historia na kuwaambia ukweli wa mambo yalivyokuwa na kuwaeleza kuwa Zanzibar ni
nchi ya watu wote na ilikuwa Zanzibar na itaendelea kuwa Zanzibar na itaongozwa
na Wazanzibar ambao wana historia ya Zanzibar.
Alisema kuwa wanaCCM wana ulezi mkubwa
katika kuwaeleza vijana kuijua historia ya nchi yao sambamba na kuzingatia
silka na maadili ya Kizanzibari.
Alieleza matumaini yake kuwa tawi hilo
litatoa elimu kwa CCM, na kuwataka vijana kujitokeza kuwenda kupokea elimu ya itikadi
na kueleza kuwa mafunzo ya itikadi yanatoa elimu kubwa.
“Mafunzo ya itikadi ndiyo wanayoyafanya
vijana katika nchi za wenzetu kuwa na moyo wa kizalendo na uchungu wa nchi
yao”,alisema Dk. Shein.
Alieleza kuwa siri kubwa ya maendeleo ya nchi zinazoendelea ni
mafanikio waliyoyapata katika kuwakuza vijana wao wakiwa na mapenzi na moyo wa
kizalendo kwa nchi zao popote walipo.
Dk. Shein alisema kuwa CCM ni chama
makini chenye uwezo wa kuongoza watu na kusisitiza kuwa kila mmoja ana ruhusa ya
kusema kwa vile kila mmoja ana mdomo wa kusema lakini cha ulazimu ni kuangalia
anachosema nini na anasema wapi jambo ambalo CCM hilo inalijali.
Sambamba na hayo, Makamu Mwenyekiti huyo
wa CCM Zanzibar alitumia fursa hiyo kuwaeleza wanaCCM kuwa wanajukumu la
kuwashawishi wale wachache ambao hadi sasa hawajafikia maamuzi ya busara ya
kukichagua Chama Cha Mapinduzi ili
kiendelee kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo ya haraka nchi yao.
Mapema Mwenyekiti wa ujenzi wa Tawi hilo Ahmada
Yahya Abdulwakil alisema kuwa Tawi hilo ni
miongoni mwa matawi ya CCM yaliyomo katika Mkoa wa Magharibi Wilaya ya Dimani
kichama, Jimbo la Kiembesamaki.
Alisema kuwa chimbuko laTawi hilo ni
utekelezaji wa maelekezo ya katiba ya CCM Ibara ya 31 (2) kinachosema kuwa Tawi
litafunguliwa tu iwapo mahala hapo panapohusika kuwa na wanachama wanasiopungua
50 na wasiozidi 600.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa Wazo la
ujenzi wa Tawi hilo lilibuniwa na wanachama wa CCM wa tawi hilo baada ya kuona
ipo haja ya kutanua wigo ili kukiwezesha chama hicho kutekeleza vyema majukumu
yake katika eneo hili kwa urahisi zaidi. Aidha, wazo hilo ni utekelezaji wa
mradi wa kuimarisha CCM Awamu ya Tatu.
Alisema kuwa kabla ya kuanzishwa kwa tawi
hilo wanachama wa tawi la CCM kwa mchina walikuwa wakitumia tawi la CCM,
Tomondo na wakati wakiwa katika heka heka za dhamira za ujenzi wa tawi hilo
walikuwa wakifanyia shughuli zao mbali mbali za kichama kwa mwanachama mwenzao
muanzilishi bi Khadija Kassim Shamte.
Walitoa shukurani kwa Balozi Seif Idd kwa
kupatikana eneo hilo ambapo shughuli za ujenzi zilianza rasmi Septemba 28 mwaka
2013 ujenzi mara tu baada ya kubapatikana hati miliki ambapo jiwe la msingi
liliwekwa Disemba 27 mwaka 2014.
Katika ujenzi huo wanachama mbali mbali
wa CCM walichagia akiwemo Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed
Shein ambaye alitoa T.shs 17,000,000 ambazo zilisaidia kumalizia ujenzi wa Tawi
hilo,na Balozi Seif Idd ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM alitoa T. shs.
5,800,000 pamoja na Tsh. milini 4 kwa ajili ya kununulia mbao za kuezekea.
Ahmada alisema kuwa hadi kumalizika kwa
jengo hilo jumla ya T.shs. milioni 79.340,000 zimetumika.
Nae Mwenyekiti wa Tawi la Mombasa
Kwamchina, Bi Subira Kahalan Urua alitoa
pongezi wka Kamati ya Ujenzi na wananchi na wanachama wote waliohuidhuria pamoja na waliochangia ujenzi huo.
Nae Balozi Seif Ali Idd, Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar alitumia fursa hiyokutoa shukurani kwa wanaCCM wa Tawi la
Mombasa Kwamchina na kuwapongeza kwa michago yao na kuwasisitiza wanaCCM
kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura
Mwenyekiti wa Mkoa wa Magharibi Yussuf
Mohammed alisema kuwa ufunguzi huo ni sehemu ya ushindi wa chama hicho.
Rajab Mkasaba,
Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
0 Comments