Na Haji Nassor, Pemba
Walishasema wahenga kuwa …..lugha nzuri hutoa nyoka pangoni…. lakini wengine wakasema…. nyimbo mbaya haimbiwi mtoto…….
Kwa asiejua maana, anaweza kuona kama misemo hiyo haina maana yoyote, na pengine kwa vile hawajui maana halisi.
Wapo wengi wamekuwa wakipuuza maneno yaliosemwa na waliotutangulia na hatiame kukumbana na majanga wasioyatarajia.
Wasomi na vijana waleo waliozaliwa ndani ya mtandao wa komputa wala hujifanya hawana shida tena na misemo ya zamani, lakini mwisho wa siku huharibikiwa.
Zanzibar kokea kuanza kwa heka heka za kampeni, tunaweza kusema haikua shuwari sana, maana hata unapoona kuna sioutofahamu ya maneno, hapo ujue lipo neno.
Lakini kazi kubwa iliofanywa na wazanzibari wenyewe, ikiwa ni pamoja dua za kucha kuchwa, basi zilisaidia sana kumaliza kampeni kwa salama na amani.
Ijapokuwa matukio hapa na pale yaliripotiwa, lakini kwa anaefahamu chaguzi nne zilizopita, wenyewe wazanzibari walisema kampeni zimeisha salama.
Hata mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya AFP Said Soud Said na hata mwenzake wa ADC Hamad Rashid Mohamed na viongozi wengine kadhaa walisifu kampeni zilizvyokuwa.
Kisha taifa la Zanzibar likaingia katika hatua muhimu hapo Oktoba 25 mwaka huu, kwa wananchi kuwachagua viongozi wao watano, kwa maana ya wabunge, wawakilishi, madiwani na marais wawili.
Waandishi wa habari na vyombo vyambo, wapo wadau waliosifia kwamba walifanya kazi zao vyema, na ndio maana kampeni ziliisha salama.
“Word choice’ kwa maana ya uchaguzi wa maneno ndio uliofanywa na waandishi hao, hali iliopelekea kipindi cha kampeni kumaliza bila ya vyombo hivyo kuchochea.
Sakata la kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ‘ZEC’ Jecha Salim Jecha, linaendelea kuchukua sura mpya siku hadi siku, huku kila kundi likitoa msimamo wake.
Kwa mfano Chama cha Mapinduzi CCM, ADC, AFP, JAHAZI-ASILIA, chama cha wananchi CUF, ambapo hata kwa Tanzania bara zipo taasisi zilizotoa matamko yao.
Mote humo, waandishi wa habari wamekuwa karibu kufuatilia, kurikodi, kupiga picha na wengine kuzichapisha habari hizo kwa mujibu wa vyombo vyao.
Naamini vyombo vya habari navyo vinafanya wajibu wa kuwahabarisha wananchi, kila kinachojiri ili kuwapa haki yao ya kikatiba.
Sasa suala la uchaguzi wa maneno, kwa waandishi wa habari katika kipindi hiki ni muhimu, vyenginevyo wanaweza kuwa kikwazo katika kuivuusha Zanzibar salama.
Tunashuhudia waandishi wa habri wamaekuwa hawana uweledi wa uchaguzi wa maneno, na wanapopata taarifa, huamua kuzirusha hewani kama zilivyo.
Tena haya hufanywa na hata vyombo vya ndani, ambapo wahariri, waandishi na wapiga picha wao ndio wanaishi Zanzibar, kwa vyombo vya magharibi, wengi hatushangai sana.
Afisa kutoka MCT afisi ya Zanzibar Shifaa Said, amenukuliwa akisema mara kwa mara kwenye mafunzo ya waandishi wa habari, kwamba uchaguzi wa maneno ni jambo la lazima.
“Iweje uliemuhoji au alietoa tamko na kutumia lugha za kuashiria uvunjifu wa amani na lichapishwe au litangaazwe vile vile’’,alihoji Shifaa.
Jengine ambalo amekuwa akilitamka, ni kuona kama mkuu wa taasisi ametoa lugha za vitisho, huwa limeishia kwenye mkutano huo, na mwandishi akiamua kulitangaaza huwafikia walio wengi kwa muda mfupi.
Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa Habari Pemba, (PPC) Said Mohamed Ali, anasema waandishi wa habari kwa vile ni kioo cha jamii, waelewe hata uteuzi wao wa maneno uwe wa kioo.
“Hakuna haja wala mantiki kwa kila analosema kiongozi cha chama au serikali, lazima mwandishi wa habari alichapishe kwenye chombo chake, maana anaweza kuwatikisha wasomaji wake’’,alifafanua.
Yeye alipingana vikali na habari za hivi karibuni, zinazotolewa hewani na waandishi wa habari, wanaohudhuria mikutano inayoandaliwa na viongozi wa vyama bila ya kupunguza makali.
Mwandishi mstaafu wa ZBC Ali Khatib Chwaya, yeye anaona wandishi wa habari lazima wachague lugha, na sio busara kuona kila linalosemwa linachapishwa.
“Kalamu zetu ndio ambazo zitaivusha Zanzibar salama au kuitumbukiza kwenye machafuko, kama waandishi hawakuwa makini kwenye uchaguzi wa maneno’’, alisema.
Lakini pia aliwageukia wahariri ambao ndio wenye mamlaka ya kuichapisha habari, na wao kama wakichanganya ushabiki wao kwenye kipindi hichi, wanaweza kuwa sehemu ya mbadiliko.
Khatib Juma Mjaja, nae anasema suala la uchaguzi wa maneno ni jambo jema, ili kutowalisha wananchi habari ambayo ni sumu.
“Lakini pamoja na uchaguzi wa maneno, wasiwe wanakurupuka wanapoandika habari zao, maana vyombo vya habari, vinaaminika sana’’,alishauri.
Aidha mwandishi huyo nguli kisiwani Pemba, alisema maneno kama ‘inaaminika’ inasemekana’ ‘taarifa zilizopo au hata kuwatumia wanasheria na wasomi ni jambo jema.
Kubwa aliwaataka waandishi wa habari katika kipindi hichi Zanzibar ikiwa katika siuntafahamu ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi Mkuu, wasijiegemeze upande wowote.
Meneja wa redio jamii Mkoani Ali Abass Omar, yeye aliwashauri waandishi wa habari wa Zanzibar, kutoegemea upande wowote wanapoandika habari zao.
“Maadili, miiko na sheria za kazi zao lazima ziwe mbele, na kinyume chake na bila ya kujali mazingira ni hatari, maana wananchi wanaviamini sana vyombo vya habari’’,alishauri
Uchaguzi wa maneno kwa waandishi wa habari ndio ambao utawaweka wananchi ambao wengi wao hawajaamini kwamba nchi imeshatulia na hasa waposikiliza vyombo vya habari.
0 Comments