Na Haji Nassor, Pemba
SHIRIKA la Huduma za Maktaba Kisiwani Pemba, limeanza kutekeleza agizo la Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, la kulitaka shirika hilo, kutanua huduma zao hadi vijijini, ambapo tayari hivi karibuni wilaya ya Micheweni kumefanyika uzinduzi wa tamasha la usomaji vitabu.
Uzinduzi wa tamasha hilo, uliambatana na shindano la usomaji wa vitambu mbali mbali uliohusisha skuli kadhaa za msingi na sekondari za wilaya hiyo, zoezi lililofanyika mara baada ya uzinduzi uliofanywa Afisa Mdhamini wizara ya Elimu Pemba Salim Kitwana Sururu.
Akisoma hutuba kwa niaba ya Afisa Mdhamini huyo, Afisa uendeshaji wa wizara hiyo Salim Ali Mata, alisema sasa shirika la Maktaba linakusudia kutanua huduma za usomaji hadi vijijini.
Alisema uamuzi huo unatokana na baadhi ya wananchi na wanafunzi kushindwa kufika makao makuu ya shirika la maktaba mjini Chake chake, ambapo ni masafa ya kilomita 34 kutoka wilaya ya Micheweni.
Mdhamini huyo alieleza kuwa, suala la kujisomea kwa njia ya maktaba linawapa wasomaji utayari wa kiakili, kuwa wadadisi, na kuelewa mambo ya kielimu yanatokezea ulimwenguni.
Alieleza kuwa, ingawa kwa siku mbili za tamasha hilo hazitoshi kwa wananchi na wanafunzi kujisomea vitabu hivyo, lakini kwa kuanzia ni hatua ya uhamasishaji wakielewa kuwa utamaduni wa kusoma ndio unaotakiwa.
“Mimi naamini kuwepo hapa Micheweni kwa siku mbili hazitoshi, lakini kama vile tunawakumbusha kuwa wajenge utamaduni wa kujiosomea’’,alifafanua.
Kwa upande wake Msaidizi Mkutubi Mkuu wa Zanzibar Abdalla Omar, ameutaka uongozi wa wilaya ya Micheweni, kuangalia uwezekano wa kupatiwa eneo kwa ajili ya kujenga maktaba.
Alisema ni vigumu kwa wananchi na wanafunzi kufuata huduma hiyo makao makuu, hivyo kama wananchi wa Micheweni wanalo eneo, ni vyema wakaarifiwa ili kuanza harakati za ujenzi.
Nae Afisa elimu na mafunzo ya amali wilayani humo, Mbwana Shaame amesema ni faraja ilioje, kuona Shirika la Huduma za Maktaba, kuanza tamasha hilo wilaya hiyo.
Makamu wa Pili wa rais wa Zanzibar Mhe: Balozi Seif Ali Idd, wakati akifungua jengo jipya la Shirika la Maktaba Pemba, mwezi Januari mwaka huu, aliliagiza shirika hilo kutanua utaowaji wa huduma zake hadi vijijini.
Skuli zilizoshiriki katika shindano fupi la tamasha hilo ni Micheweni Msingi, Simai, Karume, Konde, ambapo kwa upande wa skuli za sekondari ni Micheweni, Konde pamoja na Mgogoni.
0 Comments