Tangazo
la Washindi
Washindi wa tuzo mpya ya
Mabati-Cornell ya Fasihi ya Kiafrika walitangazwa leo (Novemba 17, 2015). Lengo
kuu la tuzo hii ni kutambua uandishi bora kwa lugha za Kiafrika na kuhimiza
tafsiri kutoka lugha za Kiafrika kwa lugha nyingine, baina ya lugha za Kiafrika
zenyewe kwa zenyewe, na pia kwa lugha za Kiafrika.
Washindi wa kwanza wa tuzo hii
ni:
Zawadi ya Kwanza ya Riwaya - $5,000:
Anna Samwel Manyanza kwa Penzi la Damu
Zawadi ya Kwanza ya Ushairi -
$5,000: Mohammed K. Ghassani kwa N'na
Kwetu
Zawadi ya Pili katika utanzu
wowote - $3,000: Enock Maregesi kwa Kolonia
Santita (riwaya)
Zawadi ya Tatu katika utanzu
wowote, $2,000: Christopher Bundala Budebah kwa
Kifaurongo (ushairi)
Hiyo ni miongoni mwa miswada 65
iliyowasilishwa, na kusomwa na waamuzi
6:
Riwaya - Dk. Farouk Topan, Prof.
Sheila Ryanga na Prof. Mohamed Bakari.
Ushairi - Bi. Rukiya Harith
Swaleh, Prof. Clara Momanyi na Prof. Alamin Mazrui.
Waamuzi walisema kuwa, “
Wakitumia lugha inayovutia na iliyo muwafaka, na mara nyingine lugha cheshi,
washindi walizungumzia maswala yanayozikumba jamii za Afrika Mashariki, kama
vile utumiaji wa mihadarati na athari zake duniani; swala la jinsia – wanawake
na haki zao; na ufisadi wa kisiasa. Huu ni ukweli halisi wa Afrika katika lugha
ya Kiafrika.”
Washindi watakabidhiwa zawadi zao
katika Tamasha la Fasihi la Kwani? (Kwani? Lit Fest) litakalofanyika Desemba
3, 2015 katika Klabu ya Capital mjini Nairobi, Kenya.
Sarit
Shah, Mkurugenzi wa Mabati Rolling Mills Kenya alisema, “Kuongezeka kwa
matumizi ya Kiswahili kuwa ni lugha kuu ya mawasiliano Afrika Mashariki
hakuwezi kupuuzwa. Tunaamini kuwa lugha na tamaduni huboresha mahusiano ya
kikazi na ya kibinafsi. Hapa Safal, hasa hapa Mabati, tunajivunia kuwa katika
jamii hii inayoendelea kukua.”
Abdilatif
Abdalla, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, alisema, “Jambo la kufurahisha ni
kwamba sehemu kubwa ya miswada iliyopokewa ilikuwa ni ya kiwango cha juu. Kwa
sababu ya kanuni za tuzo hii, ni washiriki wane tu ndio wanaoweza kutunukiwa
zawadi. Hata hivyo, ni matumaini yangu kwamba hao washiriki wengine
hawatavunjika moyo, bali wataendelea kushiriki katika mashindano yafuatayo, na
kwamba baadhi yao watafarijika kwa maandishi yao kuchapishwa vitabu pia.
Yanastahili.
Mukoma Wa Ngugi,
mwanzilishi-mwenzi wa tuzo hii alisema, “Kiwango cha msaada tuliopokea
kinadhihirisha kuwa kuna uhitaji, na pia uwanja mpana, wa kuandika kwa lugha za
Kiafrika; na kuwa utamaduni wa Kiafrika wa fasihi unaweza kustawi katika lugha
za Kiafrika, na kwamba lugha za Kiafrika zinaweza kukuzwa kupitia ufadhili
kutoka Afrika kwenyewe.”
Lizzy Attree, mwanzilishi-mwenzi
mwengine wa tuzo hii alisema, “Tunawashukuru wote walioleta miswada yao katika
shindano hili, na tunatarajia kuwa tuzo ya mwaka huu itawahimiza waandishi
zaidi kushiriki katika shindano la mwaka ujao.”
Masharti ya Tuzo:
1.Tuzo itatolewa kwa muswada bora
ambao bado haujachapishwa, au kwa kitabu kilichochapishwa miaka miwili kabla ya
mwaka wa tuzo, katika tanzu za riwaya, tamthilia, ushairi, wasifu, na riwaya za
michoro. Jumla ya dola za Marekani 15,000 zitatolewa zawadi kama ifuatavyo:
Zawadi ya Kwanza ya Riwaya -
$5,000
Zawadi ya Kwanza ya Ushairi - $5,000
Zawadi ya Pili katika utanzu
wowote - $3,000
Zawadi ya Tatu katika utanzu
wowote - $2,000
2. Kitabu au muswada utakaoshinda
utachapishwa kwa Kiswahili na shirika la uchapishaji la East African
Educational Publishers; na diwani
bora ya mashairi itatafsiriwa na kuchapishwa na Africa Poetry Book Fund.
3. Sherehe ya kuwatuza washindi
wanne, itakayohudhuriwa na washindi wenyewe, itakuwa Kenya. Washindi hao
wataalikwa Chuo Kikuu cha Cornell, watakakokuwa kwa wiki moja; kisha wiki moja
nyingine watakuwa katika asasi shiriki (ya Marekani ama Afrika) mwaka 2016.
Shindano la mwaka 2016:
Washiriki wanaombwa kupeleka
miswada ambayo haijachapishwa, au vitabu (riwaya, tamthilia, ushairi, wasifu,
au riwaya za michoro), vilivyochapishwa kwa Kiswahili miaka miwili kabla ya
mwaka wa tuzo, kwa: kiswahiliprize@cornell.edu kabla ya Machi 31,
2016. Miswada ya maandishi ya nathari isipungue maneno 50,000; na ya ushairi
isipungue kurasa 60.
Waamuzi:
Waamuzi watabadilishwa kila mwaka
na kuchaguliwa na wadhamini wa Tuzo.
Tarehe Muhimu:
Tarehe ya mwisho ya kupeleka
miswada au vitabu ni Machi 31, 2016. Orodha ya kwanza itatolewa Julai 2016, na
washindi watatangazwa Oktoba 2016.
Kwa Wahariri:
Tuzo ya Kiswahili ya Mabati Cornell ya Fasihi ya Kiafrika ilianzishwa na Prof. Mukoma Wa Ngugi na Dk. Lizzy Attree
mwaka wa 2014 ili kuendeleza uandishi bora kwa lugha za Kiafrika na kuhimiza
tafsiri kutoka lugha za Kiafrika kwa lugha nyingine, pia baina ya lugha za
Kiafrika zenyewe kwa zenyewe.
Tuzo ya Mabati-Cornell:
Kwa kiasi kikubwa, tuzo hii
inadhaminiwa na Mabati Rolling Mills of Kenya (sehemu ya Kampuni ya Safal),
Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Maswala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cornell,
Idara ya Masomo na Utafiti ya Afrikana
Mabati Rolling Mills:
Mabati ni sehemu ya Kampuni ya
Safal, inayotengeneza mabati katika nchi 11 za Mashariki ya Afrika na Kusini
mwa Afrika.
Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Maswala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cornell inatoa mwongozo na kusaidia
katika kusimamia juhudi za kuzidisha shughuli za kimataifa Cornell. Lengo lake
ni kushirikiana na shule, vyuo na vituo ili kuendeleza na kutekeleza mipango
inayohusiana na shughuli za kimataifa za Chuo Kikuu hiki. Ofisi hii itaisaidia
Halmashauri mpya ya Kimataifa, ambayo mwenyekiti wake ni Makamu wa Mkuu.
Idara ya Masomo na Utafiti ya Afrikana ni Idara ya
Masomo na Utafiti ya Afrikana, mazingira
ya kielimu, ya kitamaduni na ya kijamii kwenye Chuo Kikuu cha Cornell, Ithaca.
Tovuti: http://www.asrc.cornell.edu
East
African Educational Publisher (EAEP) ni shirika mojawapo kuu la wachapishaji. EAEP linajitahidi
kuyahusisha maadili yanayoonekana kama kwamba yanakinzana; yaani kuchapisha
kazi za kiwango cha juu zinazogusia maswala ya kijamii, ya kitamaduni na ya
kiuchumi, na wakati huo huo kufaulu kufanya biashara iliyo tayari kukabiliana
na hali halisi na misukosuko ya zama za kiteknolojia.
Africa
Poetry Book Fund inaimarisha
na kuendeleza uchapishaji wa sanaa za kishairi kupitia vitabu vyake,
mashindano, warsha na semina pamoja na kushirikiana na wachapishaji, matamasha,
mawakala, vyuo, vyuo vikuu, makongamano na vikundi vingine vinavyohusika na
ushairi Afrika.
Tovuti: http://africanpoetrybf.unl.edu/
Bodi ya Wadhamini: Abdilatif Abdalla (Mwenyekiti), Mukoma wa Ngugi, Lizzy
Attree, Happiness Bulugu, Walter Bgoya, Henry Chakava, Chege Githiora, Carole
Boyce Davies, Rajeev Shah, Ngugi Wa Thiong’o – na wengine watakaotangazwa
baadaye.
Twitter: @KiswahiliPrize
Kwa Mawasiliano:
Prof. Mukoma Wa Ngugi, kiswahiliprize@cornell.edu
Dr Lizzy Attree, kiswahiliprize@cornell.edu
0 Comments