NA HAJI
NASSOR, PEMBA
MALI za
wizara ya afya zilizomo kituo cha Afya Wesha wilaya ya Chakechake Pemba, ziko
hatari kuibiwa wakati wowote, iwapo mtindo kukifungua kituo hicho na kukiwacha
wazi kwa muda, unaofanywa na madaktari hawatouwacha.
Madaktari kwenye kituo hicho,
wamekuwa na mtindo wa kikufungua kituo hicho na kisha kurudi nyumbani, hasa kwa
yule daktari aliejengewa nyumba karibu kituo hicho.
Imefahamika kuwa, utaratibu wa
kukiwacha wazi kituo hicho na kisha kurudi tena nyumbani, ndio wa kawaida kwa
madaktari hao, jambo linaloweza kusababisha wizi kwa njia rashisi.
Hayo yamegunduliwa na Kamati ya
maofisa wadhamini kisiwani Pemba, ilipofanya ziara ya kushitukia, walioifanya
kwenye Kituo hicho majira ya saa 1:38 asubuhi, ili kuangalia mwenendo wa
utendaji kazi kwenye sekta ya afya.
Akizungumza na madaktari hao baada
maofisa wadhamini hao kukitembelea kituo hicho kikiwa wazi, pasi na kuwepo
daktari yoyote, Afisa Mdhamini anaeshughulikia Utumishi wa Umma Pemba, Massoud
Ali Mohamed, alisema lazima sheria na kanuni za Utumishi wa umma zifuatwe kwa
vitendo.
Aliwaeleza kuwa mtindo wa kukifungua
Kituo hicho cha Afya na kukiwacha wazi, unaweza kuwasababishia hasara, iwapo
atatokezea muhalifu na kufanya hujuma kwenye jengo hilo la serikali.
“Tumekikuta kituo kiko wazi, sisi
tumeingia vyumba vyote viko wazi na hapana hata mlinzi, zaidi ya mama mjamzito
tuliemkuta, sasa hapo inaweza kuwa rahisi kufanyika kwa wizi’’,alifafanua.
Mdhamini huyo, alisema alipomuhoji
mama huyo mjamzito, alimueleza kuwa, ndio kawaida kwa kituo hicho cha afya cha
Wesha, kuanza kutoa huduma saa 3:00 licha ya kufunguliwa saa 1:00.
Nae Afisa Mdhamini anaeshughulia
wanawake na watoto Pemba, aliekuwemo kwenye ziara hiyo Khadija Khamis Rajab alisema
uhaba wa madatari kwenye kituo hicho isiwe sababu ya kikufungua Kituo hicho, na
kikiwacha wazi kwa madai ya machofu.
“Bora mchelewe kikufungua, ingekuwa
afadhali, kuliko kikifungua mapema na kisha mkarudi nyumbani, au kwa sababu mtu
yuko karibu anakwenda kazini, hili sio sahihi”,alifafanua.
Madaktari waliofika kituoni hapo nusu
saa baadae, waliwaeleza maofisi hao wadhamini kuwa, wamekuwa wakifanya kazi nje
ya wakati na kuondoka hapo wakiwa wamechoka.
“Tukiondoka hapa siku nyengine tumechoka,
maana tuko wachache, kazi inakuwa inapindukia muda, sasa tukifika majumbani
tumechoka na asubihi huchelewa kuja’’,alisema daktari mmoja.
Aidha madaktari hao, waliwaahidi
maofisa wadhamini hao kuwa mtindo wa kukifungua kituo hicho na kisha kuondoka,
utakoma kwani hufanya hivyo kwa dharura.
Hata hivyo wamewaomba kuhakikisha
wanalitafutia ufumbuzi tatizo la uhaba wa watendaji kwenye kituo hicho,
kwani ikitokezea mmoja amepata dharura
utoaji wa huduma husuasua.
Wakati huo huo maofisa wadhamini hao, wamemuagiza
daktari aliekifungua kituo hicho cha afya Wesha, na kikiacha wazi kwa zaidi ya
nusu saaa, kuandika barua haraka ya kujieleza sababu zilizomsukuma kufanya hivyo.
“Huyu daktari ambae amejengewa nyumba
na serikali, ili aishi karibu na Kituo cha Afya, akaamua kukifungua na kisha
kurudi kwake, mwambieni aandike barua ya kujieleza, kwa kukitelekeza
kituo”,alisema Mdhamini wanawake na watoto.
Baadhi ya wananchi wanaokitumia kituo
hicho, walisema ni jambo la kawaida, kukikuta kiko wazi, pasi na kuwepo kwa
daktari.
“Mimi juzi nilimpeleka mke wangu
machana na kufika tukakaa kwa muda mrefu, na vyumba vyote tukavimaliza
kumtafuta, hatujamuona daktari wowote’’,alifafanua Mohamed Juma Abdi.
Maryam Mohamed Ali, alisema hawaoni faida
kubwa ya kuwepo kwa kituo hicho, kutokana na madaktari waliopo kutokaa sehemu
yao ya kazi, kwa wakati husika.
“Sisi wajawazito tunapokwenda na
watoto wetu kwanza usubiri daktari pengine yuko kwake, au hao wengine
hawajafika au wametoka ndio yaliopo pale’’,alifafanua .
Naibu sheha wa shehia ya Wesha Haji
Mohamed Ali, alikiri kuwepo kwa tatizo hilo, na kuiomba wizara ya afya kuajiri
watu wenye hamu na nidhamu ya kazi.
“Kituo cha afya kipo na dawa zipo,
lakini ukifika mara kwanza daktari mmoja hayupo, mwengine kwenda nyumbani hili
lazima lishughulikiwe ili wananchi waone faida ya kuwepo kwa Kituo
hicho’’,alishauri sheha huyo.
Safia Ali Kwale (50), alisema mwaka
jana alipokwenda kwenye kituo hicho alipata huduma mzuri na hakuona mashaka
yoyote kwa madaktari hao.
“Mimi sio mara nyingi kwenda kituo
chetu cha afya, lakini nilipokwenda hawajanidharau na nimewakuta juu ya viti
vyao tayari kwa kuhudumia wananchi’’,alifafanua.
Uchunguuzi uliofanya na mwandishi wa
habari hizi, umebaini kuwa kituo hicho cha afya kinadaktari mmoja mzalishaji,
mmoja wa kawaida na kukosekana kwa odali jambo linalotajwa kuwapa kazi ya ziada
watendaji waliopo.
Katika siku za hivi karibuni kamati
ya maofisa wadhamini Pemba, imekuwa ikiandaa ziara ya kushitukizia kwenye
wizara, taasisi na mashirika ya umma, ili kuangalia uwajibikaji ukiwemo wa muda
wa uingiaji na utokaji wa kazini.

0 Comments