6/recent/ticker-posts

vituo vya Afya vinavyoendelea kujengwa katika Visiwa vya Unguja na Pemba vitasaidia kuimarisha huduma za Afya -Mazrui

 Na.Omar Abdallah -Wizara ya Afya.

WAZIRI wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui amesema vituo vya Afya vinavyoendelea kujengwa katika Visiwa vya Unguja na Pemba vitasaidia kuimarisha huduma za Afya zikiwemo huduma ya mama na mtoto.

Hayo ameyaeleza wakati alipofanya ziara maalaum ya kukagua maendeleo ujenzi wa vituo vya Afya vinavyoendelea kujengwa katika maeneo ya Magomeni Wandarasi, Sebleni, na Tunguu.

Waziri Mazrui amesema Wizara ya Afya imeridhishwa na kasi ya ujenzi unaoendelea wa vituo hivyo na kumaliza kwa wakati uliopangwa ili wananchi wapate huduma za Afya kwa ufanisi.

Amesema ujenzi huo umepangwa kukamilika Mwezi Novemba jambo litakaloipa nafasi Wizara ya Afya kuandaa utaratibu wa kupeleka vifaa tiba, madaktari ili kutoa fursa ya kuanza kutoa huduma za matibabu ziatakazoendelea kuimarika hadi pale vitakavyofunguliwa Januari 2026.

Amesema lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuimarisha huduma ya Afya ya msingi ili kuona wananchi wanafikiwa na huduma hizo kwa ukaribu na kwa wakati unaostahiki na kupunguza msongamano katika Hospitali za Wilaya na Mkoa.

Aidha amesema vituo vyote vinavyojengwa Unguja na Pemba vimezingatia mahitaji ya huduma mbali mbali zikiwemo za uchunguzi, upasuaji, mama na mtoto pamoja maabara ili wananchi wasipate usumbufu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya Ufundi na Miundombinu ya Afya Wizara ya Afya Zanzibar Amina Mohamed Habib amesema kazi ya ujenzi ya vituo vya Afya inaendelea vizuri na kuwataka wakandarasi kuongeza kasi zaidi katika ujenzi wa vituo hivyo ili kumaliza kwa haraka hasa vituo vilivyopo mjini.

Amesema kufuatia kuanza ukarabati na utanuzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mnazimmoja unaotarajia kuanza hivi karibuni wakandarasi wanatakiwa kukamilisha ujenzi huo hasa katika maeneo ya mjini.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments