6/recent/ticker-posts

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Ahutubia Maadhimishi ya Siku ya Ukimwi Duniani Ukumbi wa Idrisa Abdulwakil Kikwajuni

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Viongozi wa Serikali, Watendaji kutoka Tasisi mbali mbali na wananchi waliofika katika hafla ya Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR ) Tarehe 01.12.2025

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema kwa zaidi ya miongo mitatu Zanzibar imepiga hatua kubwa na kufanikiwa kudhibiti kiwango cha maambukizi ya Virusi vya  Ukimwi na kuwa chini ya asilimia moja.

 

Ameeleza hayo katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani yqloyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.

 

Amesema Zanzibar imefanikiwa kupunguza maambulizi mapya ya maradhi ya Ukimwi kutoka watu 362kwa mwaka 2020 hadi kufikia watu 211 waliopata maambukizi mapya kwa mwaka 2025 jambo lililosaidi kupunguza vifo vitokanavyo na maradhi hayo kutoka vifo 230 kwa mwaka 2020 hadi vifo 115 kwa mwaka 2025.

 

Mhe. Hemed amefahamisha kuwa Serikalini ya Mapinduzi ya Zanzibar imeandaa mpango maalum unaojuulikana kwa jina la "Mpango endelevu wa kupambana na Ukimwi Zanzibar " wenye madhumuni ya kuhakikisha mapambano dhidi ya Ukimwi yanakuwa endelevu ili kufikia  lengo la kumaliza Ukimwi ifikapo 2030.

 

Aidha, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Serikali itahakikisha Sheria na Sera zote zinazingatiwa na zinalindwa dhidi ya ubaguzi na kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya unakuwa wa haki kwa wote bila ya ubaguzi.

 

Sambamba na hayo amesema licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika mapambano dhidi ya Ukimwi bado kuna changamoto zinazohitaji nguvu, ya pamoja kuzishughulikia ikiwemo upungufu wa rasilimali fedha, unyanyapaa na kuwepo kwa tabia hatarishi miongoni mwa vijana.

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewahakikishia watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi kuwa Serikali Inayoongozwa na Rais Dkt . Hussein Mwinyi itazifanyia kazi changamoto zilizowasilishwa na Jumuiya ya ZAPHA+ ikiwemo kuongezwa Bajeti kwa ajili ya upatikanaji wa dawa na vipimo kwa wagonjwa wa Ukimwi lakini pia kuwezesha harakati za Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi nchini.

 

Mhe. Hemed amewasihi wananchi kutowanyanyapa na kuwabagua watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi kwani kufanya hivyo ni kudhorotesha jitihada za Serikali  za kumaliza maambukizi mapya ya Ukimwi.

 

Ametoa wito kwa kwa Taasisi mbali mbali, wadau na jamii kwa ujumla kushirikiana kwa pamoja katika kuhamasisha kampeni za mabadiliko ya tabia, kuongeza ubunifu na upatikanaji wa fedha na vifaa ambavyo vikitumika kwa ufanisi lengo la kumaliza Ukimwi Zanzibar litafikiwa.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Ukimwi Dkt. Ali Salim Ali amesema juhudi za kuzuia maambukizo ya Virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto zimezidi kufanikiwa kwa  kuonesha maendeleo chanya ya maambukizo yaliyo chini ya asilimia mbili  ikiwa ni hatua ya kufikia lengo la  kumaliza maambukizo ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

 

Dkt. Ali amefahamisha kuwa program za kuyafikia makundi maalum zimeimarishwa kwa kupatiwa elimu, ushauri nasaha, upimaji wa VVU na kuunganishwa na huduma za tiba ambapo jumla ya watu 6,421 wa makundi maalum wamefikiwa Unguja na Pemba.

 

Aidha, katika  kuhakikisha usawa wa upatikanaji wa huduma kwa watu wanaoishi na virusi vya ukimwi hasa wanaume  ushirikiano katika jamii unazidi kuimarishwa ili kuondoa vikwazo vinavyowazuia  wanaume kupata huduma muhimu za matibabu ya VVU.

 

Akisoma risala ya watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Zanzibar  Bibi Sara Abdi Mwita amesema kutokana na Mashirika wafadhili kusuasua katika kutoa misaada hasa kwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi wanaiomba Serikali kuliangalia suala la dawa za ARV kuwekwa katika bajeti ya serikali ili huduma hio iendelee kuwa endelevu kwa wagonjwa wa Ukimwi.

 

Amesema wagonjwa wa Ukimwi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbali mbali katika sehemu za utowaji wa huduma za kijamii hivyo wameomba kusaidiwa  waweze kutambulika kuputia mifumo mbali mbali ya utoaji wa huduma hasa hospitali ili waweze kupatiwa huduma pasipo ba usumbufu wa aina yoyote.

 

Sambamba na hayo Bi. Sara amesema katika kukabiliana na mapambano dhidi ya ukimwi serikali inapaswa kuanzisha mfuko maalumu wa HIV ambao utakabiliana na upungufu wa fedha kwa ajili upatikanaji wa  huduma muhimu kwa watu wanaoishi na Ugonjwa wa Ukimwi.

 

Siku ya Ukimwi duniani huadhimishwa kila ifikapo tarehe O1 Disemba ya kila mwaka ambapo kauli mbiu ya mwaka huu 2025 inasema Tuvishinde vikwazo vya kisedha, tuimatishe mapambano ya Ukimwi.

 

Imetolewa na kitengo cha Habari ( OMPR )

Leo tarehe 01 / 12 / 2025

Post a Comment

0 Comments