6/recent/ticker-posts

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla Amefunga Mafunzo ya Viongozi Wakuu wa SMZ

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akimkabidhi cheti cha ushiriki Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ndugu Abeda Rashid Abdala katika ufungaji wa Mafunzo ya Awali kwa Viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha  IIT Madras Bweleo Wilaya ya Magharibi " B" Unguja.

Makamu wa pili wa rais Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza wakati wa ufungaji wa Mafunzo ya Awali kwa Viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha  IIT Madrasa Bweleo Wilaya ya Magharibi " B" Unguja.

 Picha na Kitengo cha Habari (OMPR).

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewataka  viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuyatumia vizuri mafunzo waliyopatiwa ili kuweza kuleta tija na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Ameyasema hayo wakati wa ufungaji wa Mafunzo ya Awali kwa Viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha  IIT Madrasa Bweleo Wilaya ya Magharibi " B" Unguja.

Amesema mafunzo waliyopatiwa  kutawasaidia katika kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa wakizingatia kuwa lengo la kupewa dhamana za kuongoza wizara zao ni kuwatumikia wananchi si vyenginevyo.

Mhe. Hemed amesema kiongozi bora ni anaekubali kutenga muda wake kujifunza na kujiendeleza kielimu ili kuweza kufanya kazi kwa kutumia vyema taaaluma yake kwa kuziletea maendeleo Wizara na Taasisi wanazoziongozi.

Katika kufikia adhma na malengo ya Rais Dkt. Hussein Mwinyi ya kuwaletea Wazanzibari maendeleo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka viongozi hao kufanya kazi kwa kufata sheria, kanuni na taratibu za utumishi ili kufikia malengo ya serikali ya kutoa huduma bora kwa wananchi wote.

Ameitaka Wizara ya Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala bora kupitia chuo chake cha Utawala wa Umma ( IPA ) kuendelea kutoa kumafunzo yatakayowakumbusha viongozi hao katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.

Amewasisitiza viongozi waliopatiwa mafunzo hayo kufanya kazi kwa uzalendo, ubunifu na kushirikiana ili kutoa matokeo chanya ya mafunzo hayo.

Kwa upande wake katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Muhandizi Zena Ahmed Said amewataka viongozi hao kushirikiana na watendaji wao katika wizara zao ili kufikia malengo ya serikali ya kuwapatia huduma zilizo bora wananchi wote wa Zanzibar.

Mhandisi Zena amewahimiza viongozi hao kuendelea kusoma vitabu vyenye kuonesha miongozo na taratibu  za kazi ili kuweza kufanya kazi kwa ufanisi wa hali ya juu na kuweza kufikia malengo ya serikali ya awamu ya Nane ( 8 )

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wenzake waliopatiwa mafunzo hayo waziri wa ( OR ) IKULU Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum amesema mafunzo waliyopatiwa yatawasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi  na kuahidi watayafanyia kazi kwa vitendo ili kuleta mabadiliko chanya katika maeneo yao ya kazi.

Mafunzo hayo wa siku mbili yameandaliwa na chuo cha Uongozi wa Umma Zanzibar ( IPA ) yaliyolenga kuwakumbusha viongozi wa Umma wajibu wao katika Wizara na Taasisi wanazoziongoza pamoja na kuwaongezea ari na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao. 

Imetolewa na kitengo cha Habari ( OMPR )

Leo tarehe  13 / 12 / 2025

Post a Comment

0 Comments