WAZIRI wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji, Mhe. Shaaban Ali Othman, amesema Serikali inakusudia kuwafikia Vijana wote wa Mjini na Vijijini ili kuwaletea maendeleo kiuchumi na kijamii.
Mhe. Shaaban, ameyasema hayo wakati akizungumza katika Mkutano wa Wadau wa Maendeleo ya Vijana huko katika Ukumbi wa Skuli ya Utalii, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Kampasi ya Maruhubi.
Amesema Serikali kupitia Wizara hiyo, inaendelea kuimarisha na kukusanya Takwimu za Vijana Nchini ili kubaini changamoto na fursa zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi kulingana na Takwimu halisi.
Aidha amesema Serikali, itaendelea kushirikiana na Wadau mbalimbali wa Maendeleo ya Vijana ili kuhakikisha mawazo na michango yao, yanatumika katika kuwawezesha, kujiajiri au kuajiriwa.
Mbali na hayo, amezitaka Taasisi za kiraia, zinazohusiana na masuala ya Vijana, kuhakikisha zinatunza kumbukumbu za miradi wanayotekeleza na kuwasilisha ripoti za utekelezaji mara kwa mara ili ziweze kufanyiwa kazi.
Kwa upande mwengine Mhe. Othman ameahidi kuwa Serikali haitosita kuzichukulia hatua Taasisi zitakazokwenda kinyume na malengo iliojipangia.
Nae Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Salama Mbarouk Khatib, amesema Wizara, itahakikisha kuwa ajira zinazozalishwa na kampuni na Taasisi binafsi zilizopo Zanzibar, zinatoa kipaumbele kwa Vijana wazawa, ili wazidi kunufaika na rasilimali za Nchini yao.
Hata hivyo amewasisitiza Vijana kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia kwa kuwa ni nyenzo muhimu ya kufikia maendeleo ya haraka.
Nao baadhi ya Vijana walioshiriki katika Mkutano huo, wamesema ili Vijana waweze kunufaika na mikopo inayotolewa ni muhimu kupunguzwa masharti yaliowekwa kwani wengi wanaikosa kutokana na kutokuwa na Hati kama vile ya Viwanja na nyumba.

Imetolewa na kitengo Cha Habari, WVAU.




0 Comments