Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kufanya mabadiliko na mageuzi makubwa katika Taasisi ya yaraka na kumbukumbu ili kuzidisha ufanisi katika utendaji kazi hasa katika utunzaji wa nyaraka na kumbukumbu za nchi.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla wakati akiweka jiwe la msingi katika jengo la Taasisi ya nyaraka na kumbukumbu lililopo Kilimani Zanzibar.
Amesema jengo hilo litakapo kamilika litaweza kukidhi mahitaji ya sasa na ya muda mrefu kutokana na kusanifiwa kwa kuzingatia mifumo ya kiusalama, matumizi ya tehama na matumizi mbali mbali kwa watumishi pamoja na wananchi watakaofika kwa ajili ya kupatiwa huduma.
Amesema katika kufika malengo ya kutunza nyaraka na kumbukumbu kwa njia kidijitali ni lazima kuwasomesha watendaji wa Taasisi hio ili kuweza kuwa na wataalamu wabobezi wanaoweza kufanya kazi ya utunzaji wa Nyaraka na Kumbukumbu kulingana na matakwa ya Kitaifa na Kimataifa.
Mhe. Hemed amefahamisha kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono na kutoa kila aina ya Ushirikiano katika kuhakisha Zanzibar inasomeka katika ramani ya Kimataifa kwenye masuala ya Nyaraka na kumbukumbu hasa katika kuitangaza Zanzibar kihistoria
Amesema endapo Nyaraka na kumbukumbu zitatunzwa ipasavyo zitasaidia katika ufanyaji wa tafiti mbali mmbali lakini pia kuchangia pato la Taifa zikiwa kama ni kivutio kimojawapo cha watalii wanaotembelea Zanzibar.
Amewataka wafanyakazi wa Taasisi ya Nyaraka kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu mkubwa katika kuzisimamia na kuzitunza nyaraka na kumbukumbu za Taifa ambapo amewaahidi kuwa Serikalini itaendelea kuwaangalia kwa karibu zaidi watumishi wa Taasisi hio ili waweze kufanya kazi zao kwa uweledi na ufanisi zaidi.
Sambamba na hayo amemuagiza Mkurugenzi wa wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA ) kusimamia jengo hilo ili mkandarasi kampuninya ZECCON aweze kukamilisha kazi hio kwa wakati uliopangwa na endapo atashindwa kukamilisha ujenzi huo kwa wakati atakuwa amejiondolea fursa ya kufanya kazi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika ujenzi wa miradi mengine mbali mbali inayoendelea kujengwa nchini.
Nae, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Ikulu Dkt. Saada Mkuya Salum amesema Taasisi ya Nyaraka na kumbukumbu ni nyenzo na hazina muhimi inayoakisi maendeleo katika nchi yoyote ile duniani jambo lililosukuma kujengwa kwa jengo la kisasa la kuhifadhia kumbukumbu na Nyaraka Zanzibar.
Dkt. Mkuya amesema Afisi ya Rais Ikulu ipo katika hatua za mwisho kukamilisha Sera ya Nyaraka na kumbukumbu ambayo itasimamia masula yote ya utunzaji wa Nyaraka na kumbukumbu, kuangalia vipaombele vya watumishi pamoja kubadilisha Taswira ya Taasisi hio kwa kufanya kazi kidijitali ili kuzidisha usalama zaidi katika kazi zao.
Akisoma taarifa ya kitaalamu kuhusu ujenzi wa mradi wa Jengo la Nyaraka na Kumbukumbu, Katibu Mkuu Afisi ya Rais Ikulu ndugu Saleh Juma Mussa amesema ujenzi wa jengo hilo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM na ahadi za Mhe. Rais wa Zanzibar alizozitoa katika kampeni za achaguzi ambapo aliahidi kuboresha maslahi na mazingira ya wafanya kazi ili kuzidisha ufanisi katika utekelezaji wa majukumu wao.
Katibu Saleh ameeleza kuwa kwa muda mrefu watendaji wa Taasisi ya Nyaraka na kumbukumbu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya sehemu salama ya kuhifadhia Nyaraka za Taifa pamoja na ufinyu wa ofisi kwa ajili ya watumishi wa Taasisi hio ambapo Rais Dkt. Hussein Mwinyi ameamu kuiondoa changamoto hio kwa kujengwa jengo la kisasa litakaloendana na matakwa ya wakati uliopo.
Amesema jengo hilo la ghorofa tano (5) linalojengwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambalo litagharimu zaidi ya shilingi za Kitanzania Bilioni 8 litakapomalizika litakidhi vigezo vyote vinavyohitajika kuwepo katika majengo ya kuhifadhia nyaraka na kumbukumbu mbali mbali za Taifa jambo litakalotoa fursa kwa wananchi kuijua hiztoria ya nchi yao kupitia Kumbukumbu zinazoendelea kuhifadhiwa kupitia Taasisis ya Nyaraka.
Imetolewa na kitengo cha Habari ( OMPR)
Leo tarehe 28 / 12 / 2025
0 Comments