Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Na Mwandishi Wetu,KAGERA.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,George Simbachawene ameweka wazi nia ya serikali kuunganisha nguvu kazi ya wafungwa na matumizi ya teknolojia katika kilimo ili Jeshi la Magereza liweze kuendana na kasi ya matumizi ya teknolojia ya kilimo hali itakayopelekea kuongezeka kwa uzalishaji huku akiweka wazi umuhimu wa kuijumuisha sekta binafsi katika shughuli mbalimbali za uzalishaji zinazofanyika katika maeneo ya magereza mbalimbali nchini.
Ametoa kauli hiyo leo, wakati wa ziara ya kukagua shughuli za Kilimo ikiwemo shamba la mahindi katika Gereza la Kilimo na Mifugo la Kitengule lililopo wilayani Karagwe mkoani Kagera akisisitiza kuwepo kwa ulazima na uharaka wa Jeshi la Magereza kubadili mtazamo ili na kuendana kasi na maendeleo ya sayansi na teknolojia katika kilimo ikiwemo matumizi ya mbegu bora na za kisasa na matumizi ya teknolojia.
‘Lazima twende kwenye mabadiliko,tutashirikiana na SHIMA(Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Magereza, tutahakikisha kwamba tunaingia kwenye kilimo ambacho tutatumia mashine kubwa ili tuweze kuzalisha kwa ukubwa na kimsingi tuna fursa ya kuilisha nchi nzima sio kuishia kulisha wafungwa tu,tuna maeneo makubwa tutashirikisha sekta binafsi kupitia SHIMA lakini pia tunataka Kwenda kwenye kilimo cha kidijitali kitakachofanya tutoke na tulime maeneo makubwa tuliyonayo kwa tija kubwa zaidi,nafahamu kuna jitihada zilianzishwa na wenzangu nataraji kuanzia walipoishia.’ Amesema Waziri Simbachawene.
Akizungumza wakati akisoma taarifa ya kilimo na mifugo, Mkuu wa Gereza hilo, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Mikael Mafwele ameweka wazi malengo yao sambamba na changamoto wanazokutana nazo ikiwemo upungufu wa mvua, wanyama waharibifu wa mazao ikiwemo nguruwe pori na nyani ambao uharibu mazao.
‘Hapa tuna ekari 200 kwa ujumla wake lakini tumelima ekari 160 kumekuwepo na changamoto ya uchelewaji wa mvua ya kutosha hali inayopelekea kulima eneo dogo sambamba na kiwepo kwa Wanyama waharibifu wa mazao lakini tunaimarisha ulinzi ili kukabiliana na changamoto hiyo wa Wanyama wanaoharibu mazao.’ Amesema ACP Mafwele
0 Comments