6/recent/ticker-posts

Alhajj Hemed Suleiman Amewashukuru Waumini wa Dini ya Kiislamu na Wazanzibari Kwa Ujumla Kwa Kuendelea Kuilinda Amani Iliyopo Nchini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla akiwasalimia waumini wa dini ya kiislam katika Masjid Abdalla Rashid uliopo Uwanja wa Ndege wa zamani Wilaya ya Magharibi " B" Unguja  baada ya Swala ya Ijumaa.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR )Tareh 16.01.2026

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amewashukuru Waumini wa dini ya kiislamu na wazanzibari kwa ujumla kwa kuendelea kuilinda amani iliyopo Nchini.

Ameyasema hayo alipokuwa akisalimiana na waumini wa dini ya kiislam baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika masjid Abdallah Rashid Kiembesamaki Uwanja wa Ndege wa Zamani Wilaya ya Magharibi “ B”  Unguja.

Amesema kila mwananchi kwa nafasi yake ana wajibu wa kuilinda na kuitunza amani iliyopo nchi  hasa katika miezi mitukufu jambo ambalo litaisaidia serikali kufanya mambo ya kimaendeleo pamoja na kupata fadhila kubwa kutoka kwa Allah ( S.W).

Alhajj Hemed amefahamisha kuwa kila muislam na  mwananchi wa Zanzibar wana wajibu wa kufahamishana juu ya umuhimu wa kuitunza amani ambayo ndio chanzo kikubwa cha maendeleo yaliyopo nchini.

Sambamba na hayo, amewasisitiza wazanzibari kutokubali kurubuniwa na watu wachache wasioipendelea mema Zanzibar wenye nia ya kuchafua amani na utulivu uliopo nchini jambo ambalo litachangia kukosekana kwa maendeleo nchini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema uislamu unasisitiza umoja na mshikamano hasa katika harakati za kimaendeleo hivyo inapaswa kuyafanyia kazi kwa vitendo mafundisho hayo hasa katika suala zima la kuwatumikia wananchi.

Akitoa hutuba ya swala ya Ijumaa Ustadh Abdalla Said Ali amewataka        waumini wa dini ya kiislam kujikurubisha kwa Allah  ( S.W ) wakati wote kwa kufanya Ibada kwa wingi ikiwemo na kuacha makatozo yake ili kuendelea kupata radhi zake hapa dunia na akhera.

Ustadhi Abdalla  amewasisistiza waumini hao kuendeleza mshikamano uliopo baina yao pamoja na kuiombea duwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na viongozi wake ili waweze kutimiza malengo yao ya kuwaletea wazanzibari maendeleo.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)

Leo tarehe….16 .01.2026

Post a Comment

0 Comments