Na Abdala Sifi- WMJJWM Dodoma.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameitaka Sekretarieti ya Uratibu wa Mpango wa Kitaifa wa Kupinga Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA II) kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu yake ili kuhakikisha vitendo hivyo vinapungua nchini.
Waziri Gwajima amesema hayo tarehe 23 Januari 2026, Jijini Dodoma wakati akiendesha kikao Cha Waratibu wa MTAKUWWA II, ambacho kimefanyika kwa njia ya mtandao kwa kushirikisha Viongozi wa Wizara pamoja na Maafisa Maendeleo na Maafisa Ustawi wa Jamii wa Mikoa.
Waziri Gwajima ameeleza kwamba Wizara imeendelea kushirikiana na Wizara za Kisekta na wadau wa Maendeleo kuratibu wa MTAKUWWA II 2024/25 – 2028/29), ambao una maeneo nane ya utekelezaji yakiwemo kuimarisha Uchumi wa Kaya; Mila na Desturi; Mazingira Salama katika Maeneo ya Umma na Mtandaoni; Malezi, Msaada wa Familia na Mahusiano; Utekelezaji na Usimamizi wa Sheria na Utoaji wa Huduma kwa Wahanga na Manusura wa Ukatili.
Ameongeza kwamba ili kupambana na ukatili wa aina zote ni lazima Waratibu wa Mpango huo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi katika ngazi ya Mikoa, Wilaya, Kata na Mitaa ili kupata kuelewa dhana na majukumu ya Kamati za MTAKUWWA ngazi za Kata na Vijiji na Mitaa.
“Nawaomba wajumbe wa Kamati ya MTAKUWWA na Sekretariati yake kuimarisha mifumo ya mawasiliano na utoaji wa taarifa kwa umma, njia hii itatoa namna ya kuendelea kushughulikia changamoto zinazojitokeza, pamoja na kushirikishana mafanikio yanayopatikana katika utekelezaji”. Amesema Waziri Gwajima
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju amewaomba Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na Maafisa Ustawi wa Jamii kuweka ajenda ya kuelimisha Watendaji katika Halmashauri za Wilaya, Miji, na wadau wanaohusika utekelezaji wa MTAKUWWA ili kuwa na uelewa wa pamoja jambo ambalo litarahisisha utekelezaji wenye matokeo yanayotarajiwa.
Naye Afisa maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mara Neema Ibamba ameishukuru Wizara kwa kuwakutanisha wadau muhimu katika utekelezaji wa MTAKUWWA II kwani itasaidia kuweka sawa mipango na mikakati ya utekelezaji wa mpango huo na kuwa na uelekeo mzuri kwa matokeo chanya.
%20(1).jpeg)
0 Comments