6/recent/ticker-posts

Kampuni ya Ujenzi ya **Kumpular Construction ya Uturuki yaonesha nia ya kuwekeza katika sekta ya ujenzi Zanzibar


 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), Ndg. Sultan Said Suleiman, amefanya mazungumzo na Kampuni ya Ujenzi ya **Kumpular Construction and Foreign Trade Co. Ltd** kutoka Uturuki, ambayo imeonesha nia ya kuwekeza katika ujenzi wa nyumba za bei nafuu kwa kutumia teknolojia za kisasa.

Akizungumza na ujumbe wa kampuni hiyo ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Bw. Mustafa Ozdemir, Ndg. Sultan alieleza jitihada zinazochukuliwa na Serikali kupitia Shirika la Nyumba katika kusimamia na kuendeleza miradi mbalimbali ya nyumba za makaazi. Amesisitiza kuwa ujenzi wa nyumba za kisasa ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa lengo la kukidhi mahitaji ya makazi kwa wananchi sambamba na kuimarisha mandhari na mpangilio wa miji ya Zanzibar.
Aidha, Ndg. Sultan amesema Shirika la Nyumba lina uhitaji mkubwa wa uwekezaji katika sekta ya nyumba na liko tayari kushirikiana na makampuni mbalimbali ya ndani na nje ya nchi kupitia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (Public Private Partnership – PPP). Katika muktadha huo, ameitaka Kampuni ya Kumpular kuwasilisha maombi rasmi yanayoeleza dhamira yao ya kuwekeza, ili kutoa fursa ya kubadilishana mawazo na wataalamu wa Shirika la Nyumba na kuchambua kwa kina uwezekano wa utekelezaji wa mradi huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kumpular Construction and Foreign Trade Co. Ltd, Bw. Mustafa Ozdemir, amesema kampuni yake ina dhamira ya kuwekeza katika ujenzi wa nyumba za makaazi zipatazo 3,000 kwa kipindi cha miaka minne, kwa kutumia teknolojia ya kisasa inayochanganya matumizi ya chuma, ikiwa ni sehemu ya mchango wa kampuni hiyo katika kusaidia upatikanaji wa nyumba bora na za gharama nafuu Zanzibar

Post a Comment

0 Comments