6/recent/ticker-posts

Mhe. Hemed akagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja wa Mpira wa AFCON Fumba

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman akikagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja wa Mpira wa AFCON unaojengwa Fumba Wilaya ya Magharibi "B" Unguja.




 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewahakikishia wazanzibari kuwa ujenzi wa Uwanja wa AFCON Fumba utamalizika kwa wakati uliopangwa na kutumika katika Michuano ya Afcon inayotarajiwa kufanyika Mwakani  2027.

 Ameyasema hayo katika ziara yake ya kufuatilia maendeleo ya ujenzi wa uwanja wa Zanzibar Sport City ( ZANZIBAR ARENA ) unaojengwa Fumba Wilaya ya Magharibi "B" Unguja.

 Amesema vifaa vyote kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa AFCON vimekamilika na kazi ya ujenzi inaendelea mchana na usiku ili kuhakikisha adhma ya Mhe. Rais Dkt. Hussein Mwinyi inatimia kwa uwanja huo kutumika katika Mashindano ya AFCON 2027.

 Aidha, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema ujenzi wa uwanja huo utajumuisha Uwanja mkubwa wa Mpira, uwanja wa mazoezi, uwanja wa paredi, bwawa la kuogelea, Hoteli ya nyota tano, Hospitali, kumbi za mikutano ambao unatarajiwa kuchukua zaidi ya wanamichezo Thelathini na Sita elfu  (36,000.)

 Mhe. Hemed amewataka wananchi wa Zanzibar kuzitumia fursa mbali mbali za kibiashara zitakazopatikana mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa uwanja wa AFCON Fumba .

 Hata hivyo, Mhe. Hemed amewakaribisha wawekazi kuendelea kuja kuekeza Zanzibar katika eneo la Fumba na maeneo mengine kwa kujenga  miradi mbali mbali ya maendeleo itakayosaidia kuimarisha na kukuza uchumi wa Zanzibar.

 Ameipongeza Kampuni ya ujenzi ya ORKUN group of Zanzibar na Mshauri elekezi AL-KHATMY Design and Engineering Consultancy kwa kazi kubwa wanayoifanya katika ujenzi wa miradi mbali mbali ya maendeleo hapa Zanzibar ambapo amewahakikishia kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kutoa kila aina ya mashirikiano ili kuhakikisha miradi hio inajengwa kwa ustadi na kukamilika kwa viwango vilivyokusudiwa.

 Amewata waandishi wa habari kuwa mabalozi wazuri wa kuwafikishia wananchi taarifa sahihi  juu ya ujenzi wa miradi mbali ya maendeleo inayojengwa na serikali ya mapinduzi ya Zanzibar yenye lengo la kuweka ustawi bora wa wananchi wa Zanzibar.

 Kwa upande wake Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Mhe. Dkt. Riziki Pembe Juma amemshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussein Ali Mwinyi kwa kuendelea kuipa kipaombele sekta ya Michezo kwa kuamua kujenga uwanja wa mpira wa kisasa wenye hadhi ya Kimataifa utakaotumika kwa mishindano ya Afcon 2027.

 Dkt. Riziki amewataka wananchi hasa wajasiri amali kujipanga kuutumia uwanja huo kwa kufanya biashara na kuitangaza Zanzibar kiutalii kutokana na wingi wa wageni watakaoingia nchini.

 Akizungumzia suala la matayarisho ya kuelekea mashindano ya AFCON 2027 Dkt. Pembe amesema Serikali zote mbili kupitia wizara zake za Habari zimeshaunda kamati ya pamoja ambayo inashughulikia masuala yote ya AFCON na wanaamini watafanya vuzuri zaidi hasa kwa vile tayari wana uzoefu kupitia mashindano yaliyopita ya Chaan.

 Nae Mshauri elekezi kutoka Kampuni ya Al- hatamy design and Engineering Consultancy Mhandisi ABDULHAMID MOH'D MHOMA amesema ujenzi wa  Uwanja wa Zanzibar Sports City(Uwanja wa AFCON Fumba ) unaendelea vizuri ambapo utakapomalizika utakuwa umekidhi matakwa yote ya Viwanja vya Michezo vya Kimataifa na utakuwa na uwezo wa kuchukuwa wanamichezo zaidi ya elf 36 kwa wakati mmoja.

 Mhandisi Mhoma amefahamisha kuwa ujenzi wa uwanja huo utagharimu Dola za Kimarekani Milioni 150 na matarajio yao ni kuwa ifikapo Disemba 2026 Uwanja huo utakuwa umekamilika kwa viwango vya hali ya juu na utakabidhiwa kwa serikali kwa ajili ya hatua nyengine.

 

Imetolewa na Kitengo cha Habari ( OMPR )

Leo tarehe …31 / 01 / 2026

Post a Comment

0 Comments