6/recent/ticker-posts

Mkutano wa Kikanda wa Kukabiliana na Uvuvi Haramu na Kukuza Uchumi wa Buluu



Na Sabiha Khamis Maelezo 26.01.2025

Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi inaendelea kushirikiana na wadau wa Uvuvi kutoka nchi mbalimbali ili kutokomeza Uvuvi haramu kwani hali hiypo hupelekea uharibifu wa Mazingira ya baharini. 

Ameyasema hayo Naibu Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Mhe Mboja Ramadhan Mshenga wakati akifungua Mkutano wa Kikanda wa Sauti ya Buluu (Blue Voices) huko Hoteli ya Verde Mtoni Mkoa wa Mjini Magharibi, amesema mkutano huo una lengo la kukabiliana na uvuvi haramu pamoja na kukuza Uchumi wa Buluu nchini.

Vilevile ameeleza kuwa kuboresha mashirikiano yaliopo na kuhakikisha maendeleo ya bahari yanalindwa kwa kushirikiana kupitia nchi zote zenye ukanda wa Bahari sambamba na kukuza uchumi wa buluu.

Hatahivyo amesema mkutano huo utakwenda kujadili Sera na sheria za Baharini kwa kurekebisha na kuengeza kwani ndio nguzo imara ya utekelezaji,sambamba na kuwataka wavuvi kuitumia vyema rasilimali hiyo kwa maslahi ya Taifa.

Amesema kuwepo kwa tatizo hilo kutapelekea rasilimali ya viumbe vya baharini kutoweka kama vile matumbwe samaki wadogo wadogo na kusababisha kutokea kwa mabadiliko ya tabia nchi katika bahari hizo.

Amefafanua kuwa matumaini yake kuona uvuvi unaendelea kuleta tija na manufaa katika jamii na kusaidia kuinua Uchumi wa nchi kwa kuungana pamoja katika kuweka mazingira yenye usalama katika Bahari hizo. 

Aidha Mhe Mboja amesisitiza kuwa Samaki ni rasilimali inayoisha hivyo ni vizuri wavuvi kuitunza na kuilinda rasilimali ya bahari kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Nae Msemaji wa Mradi wa Jahazi Michael Mallya amesema lengo la mkutano huo ni kukutanisha Serikali za ukanda ambao wanashirikiana katika kutumia Bahari ya hindi hususana kwa nchi za Afrika Mashariki na ukanda wa Kusini Magharibi mwa Bahari ya hindi kwa lengo la kujadili jinsi ya kutatua tatizo la uvuvi haramu kwa maendeleo ya baharini na kudumisha ushirikiano.

Amefafanua kuwa kuboresha mashirikiano yaliopo ili kuzuia changamoto za uvuvi haramu ikiwemo uvuvi unaofanywa na meli kubwa kutoka nje (deep sea), ambao husababisha kutoweka kwa Samaki katika Bahari na kuharibu miundombinu ya Bahari.

Hatahivyo amesema mkutano huo utakwenda kujadili Sera na sheria za Baharini kwa kurekebisha pamoja na kuengeza nguzo imara ya utekelezaji, sambamba na kuwataka wavuvi kuitumia vyema rasilimali hiyo kwa maslahi ya Taifa.

Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha KMKM Komodoo Azana Hassan Msingiri amesema ulinzi wa bahari ni kazi kuu ya kikosi hicho, hivyo kushiriki katika mkutano ni moja ya utekelezaji wa majukumu hayo.

Aidha ameiomba Wizara kuongeza nguvu katika kikosi hicho ili kuendelea na majukumu yao ya kulinzi wa bahari pamoja na kujitahidi katika kushirikiana katika kuimarisha ulinzi wa bahari ili kuweza kufanya kazi vizuri. 

‎Hata hivyo ameiomba Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi kukishirikisha kikosi hicho katika tafiti zinazofanyika baharini ili kuweza kulinda bahari dhidi ya uharibifu.

Mkutano huo wa siku tatu umeshirikisha wajumbe kutoka nchi mbali mbali ikiwemo Tanzania Bara, Zanzibar, Mauritius na Kenya ikiwa na kauli mbiu “Kulinda Bahari zetu Pamoja”


 

Post a Comment

0 Comments