Na.Mwandishi Wetu
WAFAMASIA
nchini wametakiwa kuandaa mpango mkakati wa usalama wa dawa katika ngazi ya Afya
ya Msingi ili kuhakikisha dawa zinahifadhiwa na kusimamiwa ipasavyo
zinapofikishwa katika vituo vyao vya afya.
Wito huo
umetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt Mngereza Mzee Miraji, alipokuwa akifunga kikao cha kutathmini mnyororo wa ugavi wa dawa
na bidhaa za afya, kilichofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, Malindi
Zanzibar.
Amesema
kuwa, kutokana na mabadiliko makubwa yaliyofanyika katika sekta ya afya kwa
kipindi cha miaka mitano iliyopita, ni wakati muafaka kwa wafamasia kuja na
mpango mkakati unaoendana na kasi ya mabadiliko katika sekta hiyo pamoja na
maendeleo ya teknolojia.
Dkt
Mngereza amesema tathmini hiyo mpya inalenga kufanya uchambuzi wa kina wa hali
halisi ya usimamizi wa mfumo wa ugavi wa dawa kuanzia ngazi ya taifa hadi
kufikia vituo vya afya vya msingi, hatua itakayosaidia kubaini changamoto na
fursa zilizopo katika mnyororo wa ugavi wa dawa.
Kwa
upande wake, Mfamasia Mkuu kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, Hidaya Juma Hamad,
amesema tathmini hiyo itaisaidia Wizara kupanga na kuamua mifumo bora ya ugavi
wa dawa ili kwenda sambamba na kasi ya ukuaji wa sekta ya afya hapa nchini.
Ameongeza
kuwa tathmini hiyo pia itafanya ufautiliaji wa suala zima la matumizi holela ya
dawa miongoni mwa wananchi na kuweka mikakati madhubuti ya kudhibiti matumizi
yasiyo sahihi ya dawa hizo, jambo litakalosaidia kulinda afya za wananchi na
kuongeza ufanisi wa huduma za afya.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la JSI (John Snow Incorporation),Dkt.Jema Bisimba, amesema mradi wa Ugavi Bora, Afya Bora unalenga kuboresha
upatikanaji wa dawa katika jamii kupitia ushirikiano wa karibu na Wizara ya
Afya Zanzibar.
Amesema
mradi huo unatekelezwa na shirika la JSI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya
Zanzibar, na umefadhiliwa na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, ukiwa na
lengo la kuimarisha mifumo ya ugavi wa dawa na bidhaa za afya kwa manufaa ya
wananchi.
Kikao
hicho kimewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya afya kwa lengo la kujadili
na kutathmini kwa pamoja njia bora za kuimarisha usimamizi wa dawa na bidhaa za
afya nchini.
Mwisho
0 Comments