6/recent/ticker-posts

NAIBU WAZIRI. WA FEDHA MHE. LUSWETULA AHIMIZA UTALII WA NDANI TANGA

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), (mwenye kofia na shati la draft) kushoto, akisikiliza maelezo kutoka kwa Mhifadhi wa Hifadhi ya Mapango ya Amboni, yaliyoko mkoani Tanga, Bw. Ramadhani Rashid, alipotembelea mapango hayo ikiwa sehemu ya utalii wa ndani alipokuwa kikazi mkoani humo.

Na Benny Mwaipaja, Tanga

Naibu Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Laurent Luswetula, ametoa rai kwa Watanzania kutembelea vivutio vya asili vilivyopo nchini ili kukuza utalii wa ndani pamoja na kuongeza pato la Taifa.

Mhe. Luswetula ametoa rai hiyo jijini Tanga alipotembelea Hifadhi ya Mapango ya Amboni, ikiwa ni sehemu ya utalii wa ndani, akiwa katika ziara ya kikazi mkoani humo.

Alisema kuwa mapango ya Amboni ni tunu ya kipekee ambayo nchi imejaaliwa na Mwenyezi Mungu, yenye kila aina ya maajabu ambayo Watanzania na wageni kutoka nje ya nchi wanatakiwa kuyashuhudia.

Wakizungumza kuhusu Hifadhi ya Mapango ya Amboni, yaliyoko chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Mhifadhi wa Hifadhi hiyo, Bw. Ramadhan Rashid na Muongoza Watalii, Bw. Muhsin Rajabu, walisema kuwa eneo hilo lina simulizi nyingi za kijiografia na historia ya wapigania uhuru wa nchi.

Aidha walisema kuwa mazingira yake ya ndani ya hifadhi yameboreshwa na kurahisisha ziara za wageni wanaotembelea eneo hilo ambalo licha ya kuwa na mapango, pia lina Wanyama wa msituni na majini wakiwemo mamba walioko kwenye mto Mkurumuzi unaopita karibu na hifadhi hiyo.

Mapango ya Amboni Tanga yana umri wa zaidi ya miaka 150, yakiwa na ukubwa wa ekari 39.5 na urefu wa mita 755 kutoka usawa wa Bahari, yanapatikana kilometa 8 kaskazini mwa mji wa Tanga ambapo tafiti zinaonesha kuwa eneo hilo lilikuwa chini ya maji kwa takriban miaka milioni 20 iliyopita.

Katika tukio lingine, Naibu Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Laurent Luswetula, alitembelea Hifadhi ya Mikoko iliyoko Jijini Tanga, na kuupongeza Uongozi wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kwa ubunifu wao na kuigeuza hifadhi hiyo kuwa sehemu ya kitega uchumi cha Taifa pamoja na kuwa eneo la utalii kwa wananchi na wageni wengine kutoka nje ya nchi wanatembelea mkoa wa Tanga.

Post a Comment

0 Comments