6/recent/ticker-posts

Wizara ya afya kujenga Hospitali ya Mkoa wa Kaskazini Unguja

Wizara ya Afya Zanzibar imetiliana Saini mkataba wa makubaliano ya Ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Kaskazini Unguja na kampuni ya Cross world Construction Limited inayotarajiwa kujengwa Mahonda Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja.
Akizungumza baada ya kukamilika utiaji Saini huo Waziri wa nchi Afisi ya Raisi Ikulu na Kaimu Waziri wa Afya Zanzibar Dkt. Saada Mkuya Salum amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa dira ya Zanzibar ya 2050 pamoja na ilani ya Chama Cha Mapinduzi inayoelekeza juu upatikanaji wa huduma bora za Afya maeneo mbalimbali nchini.
Amesema Wananchi wengi kwa sasa wamekuwa wakifuata Huduma za kibingwa katika Hospiatli ya Mkoa Lumumba, Tanzania Bara na wengine kuzifuata huduma hizo nje ya nchi hivyo kujengwa kwa hospitali hiyo kunatarajiwa kupunguza kadhia hiyo.
Ameongeza kuwa mujibu wa sensa ya watu na makaazi inaonesha kuwa Mkoa wa Kaskazini ni wa Pili kwa kuwa na idadi kubwa ya watu kwa upande wa Zanzibar hivyo ujenzi wa hospitali hiyo ni juhudi za makusudi kwa kuhakikisha wakaazi wa Mkoa huo wanafikiwa na huduma bora wakati wote.
Aidha amewaasa wajenzi wa mradi huo kuzingatia muda na viwango vinavyohitajika katika ujenzi huo vitakavyokidhi mahitaji ya wananchi Pamoja na wageni wanaofika katika mkoa huo kwa kuzingatia gharama halisi za Mradi huo.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dkt. Mngereza Mzee Miraji amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa maono ya Raisi Wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi ya kujenga Hospitali tano za Mkoa zitakazorahisisha utaoji wa hudma za Afya.
Amesema Hospitali hiyo inatarajiwa kuwa ya Ghorofa tano itakayokuwa na vitanda 200, ICU yenye vitanda 44 pamoja na kuhusisha huduma za mbalimbali za kibingwa ikiwemo huduma za dharura, Upasuaji, Usafishaji wa Figo pamoja na huduma nyengine zenye hadhi ya Hospitali ya Mkoa.
Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Cross World Construction Limited Himid Iddi Mgeni amesema dhamira kubwa ya taasisi hiyo ni kuona ujenzi huo unakamilika kabla ya wakati kwa kuzingatia viwango vinavyohitajika.
Mradi huo wa Ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Kaskazini Unguja inayotarajiwa kujengwa Mahonda unatarajiwa kutumia miezi kumi na nane.

 

Post a Comment

0 Comments