6/recent/ticker-posts

Serikali kushirikiana na jamii na Taasisi kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalum wanapata elimu sawa na wengine




Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ndg. Khamis Abdulla said amesema Serikali itaendelea kushirikiana na jamii na Taasisi mbalimbali ili kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalum wanapata elimu sawa na wengine.
Ameyasema hayo katika hafla ya ugawaji wa vifaa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum vilivyotolewa na Kampuni ya simu za mkononi Vodacom iliyofanyika katika ukumbi wa Idris Abdulwakil huko Kikwajuni, Mkoa wa Mjini Magharib, Unguja.
Amesema hatua hio ni mashirikiano mazuri kwa kushirikiana kati ya sekta ya umma na sekta binafsi kwa kuijenga jamii jumuishi kwa maendeleo ya taifa.
Amesema Wizara ya Elimu inaipongeza Kampuni ya Vodacom kwa kujitolea na kuwapatia wanafunzi vifaa vyenye ubora na vya kisasa, hivyo ameziomba Taasisi nyengine kuendelea kusaidia sekta ya elimu kwa maslahi ya taifa.
Amesema kuwa elimu mjumuisho sio chaguo bali ni haki ya msingi, na katiba ya Tanzania imesema kila mtu anahaki ya kupata elimu, afya bora, chakula na kuishi katika mazingira yaliyo bora na imara.
Aidha Bw. Khamis amewapongeza Walimu wanao wafundisha vijana hao kwani wanafanya kazi kubwa ambayo inahitaji moyo na kujitoa.
Aidha Bw. Khamis ametoa wito kwa wazazi na walezi wa watoto wenye mahitaji maalum kwa kuwalea kwa upendo, kushirikiana nao na kuwasaidia katika kutafta elimu yao na sio kuwaficha wala kuwakatisha katika masomo yao.
Mapema Meneja kutoka Kampuni ya simu za mkononi Vodacom Tanzania Bi. Sandra Oswald amesema hatua ya utoaji wa vifaa hivyo ni miongoni mwa mikakati ya kampuni hiyo ambapo wamedhamiria kuboresha maisha kwa watu wenye mahitaji maalum katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya na uchumi.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Elimu Mjumuisho na Stadi za maisha Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mwalim Juma Salim akitoa maelezo ya vifaa hivyo amesema vimegharimu takriban shilingi Milioni Mia tatu, ikiwa imejumuisha vifaa mbalimbali ikiwemo Viti mwendo vya umeme 15, Viti mwendo vya kawaida 45, karatasi za nambari 100, mashine ya ubongo (brain mashine) na visaidizi visikizi.
Imetolewa na Kitengo cha Habari, Mawasiliano na Uhusiano - WEMA.


 

Post a Comment

0 Comments