WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk. Khalid Salum Mohammed, amesema serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejizatiti kuboresha na kutanua miundombinu ya bandari nchini ili kuimarisha sekta ya usafiri na usafirishaji.
Akizungumza wakati wa kikao cha kujitambulisha kujua shughuli zinazofanywa na Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Malindi.
Dk. Khalid alisema mikakati ya serikali ni kutatua changamoto zilizopo katika bandari na kuongeza uwezo wa huduma katika maeneo mbalimbali.
Alisema hatua hiyo itasaidia kupunguza msongamano katika bandari ya Malindi na kuongeza ufanisi wa shughuli za bandari.
“Tunataka kuhakikisha kuwa huduma za usafiri na usafirishaji zinakuwa bora, huku uchumi wa nchi ukikua kwa kasi,” alisema.
Aliongeza kuwa ushirikiano na wawekezaji utaleta mabadiliko makubwa katika kuboresha huduma za bandari, na kwamba mchakato huu utaimarisha usalama na usimamizi bora wa vyombo vya majini.
Alisema miundombinu ya bandari ndiyo kiungo muhimu katika ukuaji wa uchumi, na kwamba serikali inatekeleza mikakati madhubuti kuhakikisha bandari zinakuwa salama na zenye ufanisi mkubwa.
Akiizungumzia Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), alisema ni chombo muhimu katika kuhakikisha usalama wa vyombo vya majini na kuimarisha shughuli za uchumi zinazotegemea bandari.
“ZMA inatekeleza majukumu makubwa kwa niaba ya serikali, na ndio maana tunaomba wafanyakazi wa taasisi hii wafanye kazi kwa bidii, wawe na ufanisi na kuboresha huduma kwa haraka,” alisema.
Alisisitiza kuwa ZMA inahitaji kuwa na wafanyakazi wanaohakikisha usalama wa vyombo vya majini kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuepuka ajali na matatizo mengine.
“Tunapozungumzia bandari na vyombo vya majini, usalama unapaswa kuwa kipaumbele chetu,” aliongeza.
Aidha, Dk. Khalid aliwahimiza viongozi wa ZMA kuwa na ushirikiano wa karibu na serikali ili kuhakikisha malengo ya wizara yanatekelezwa kwa ufanisi na kuleta tija kwa taifa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Wizara ya hiyo, Badria Atai Masoud, aliwasisitiza wafanyakazi wa ZMA kuwa na ushirikiano wa karibu ili kufanikisha malengo ya taasisi hiyo.
“Nidhamu na uwajibikaji ni muhimu, kazi zenu ni muhimu kwa taifa letu, na ni lazima kila mmoja ajitathmini na kuweka malengo ya kuhakikisha mafanikio ya ZMA,” alisema.
Aliongeza kuwa ni muhimu kwa wafanyakazi wa ZMA kutatua changamoto zinazojitokeza mapema, na kutosubiri ziwe kubwa ili kuepusha upotevu wa rasilimali.
“Tuna nafasi ya kuzuia matatizo kabla ya kuwa makubwa, kwa hivyo ni muhimu kila mmoja wetu kuchukua hatua mapema,” alisisitiza Badria.
Mapema akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi Mkuu wa ZMA, Mtumwa Said Sandal, alisema mamlaka imepiga hatua kubwa katika kusimamia usalama wa vyombo vya majini.
Alisema kuwa ZMA imefanikiwa kusajili meli 89 za ndani na 626 za nje, na kuwa wanatekeleza ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha vyombo vya majini vinakuwa salama na vinafanya shughuli zao kwa ufanisi.
“Tunafanya kazi kubwa katika kuhakikisha usalama wa vyombo vyote vya majini, na tunaendelea na mikakati ya kuboresha huduma na usimamizi,” alisema Mtumwa.
Ziara hiyo ya viongozi wa serikali kutembelea Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, la kuwataka mawaziri kuzitembelea taasisi zao na kusikiliza changamoto zinazozikumba, ili kuimarisha utendaji kazi wa taasisi zinazohusiana na sekta ya ujenzi na uchukuzi.


0 Comments