6/recent/ticker-posts

Skuli binafsi zina mchango mkubwa kwenye maendeleo ya sekta ya Elimu Zanzibar



Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Muhamed Mussa, ameahidi kushirikiana kikamilifu na kufanyia kazi changamoto zinazowakabili wadau wa skuli binafsi, akibainisha kuwa skuli hizo zina mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya Elimu Zanzibar.
Waziri Lela ameyasema hayo leo tarehe 17 Januari 2026, wakati wa kikao alichokiitisha na wamiliki pamoja na walimu wakuu wa skuli binafsi, kilichofanyika katika Kituo cha Walimu Kiembe Samaki, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Katika kikao hicho, Waziri amewataka wamiliki wa skuli binafsi, hususan skuli zinazofanya kazi katika majengo ya makazi, kuhakikisha wanatengeneza na kusimamia miundombinu rafiki kwa wanafunzi, ikiwemo masuala ya usafiri na mazingira salama ya kujifunzia, kwa lengo la kulinda usalama wa wanafunzi na kuifanya sekta ya Elimu kuwa mfano bora kwa sekta nyingine za maendeleo.
Aidha, ametoa wito kwa walimu wakuu na wamiliki wa skuli binafsi kuzingatia na kutii sheria, kanuni na miongozo yote iliyowekwa kwa ajili ya uendeshaji wa skuli hizo.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu – Taaluma, Dkt. Mwanakhamis Adam Ameir, amepongeza jitihada za Waziri wa Elimu kwa kuitisha kikao hicho, akieleza kuwa kimewapa fursa wadau kubadilishana uzoefu, kupokea miongozo mbalimbali, pamoja na kujadili masuala yanayohusu uendeshaji wa skuli binafsi, ikiwemo tozo za skuli na ushirikishwaji wa walimu wa skuli binafsi katika zoezi la usahihishaji wa mitihani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu Maandalizi na Msingi, Bi. Fatma Mode Ramadhan, ametoa ufafanuzi kuhusu taratibu za kufunga na kufungua skuli, akisisitiza kuwa wanafunzi wa madarasa ya tatu na chini wafungiwe skuli katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani ili kuwapa fursa ya kujifunza elimu ya madrasa kwa utulivu.
Naye Mkurugenzi wa Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Elimu Ndg. Maimuna Fadhil Abbas amewataka walimu kufanya ukaguzi wa ndani katika skuli zao ili kuunga mkono jitihada za ukaguzi wa kitaifa, sambamba na kuajiri walimu wenye sifa stahiki na kuwapatia vifaa vya kufundishia na kujifunzia, hususan katika utekelezaji wa mtaala wa umahiri unaozingatia zaidi vitendo.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Skuli Binafsi, Ndg. Kaizar, ameipongeza Wizara ya Elimu kwa mashirikiano makubwa inayoyatoa kwa skuli binafsi, na kuahidi kuwa wao kama wadau wataendelea kuthamini na kuimarisha mashirikiano hayo kwa lengo la kujenga taifa imara kupitia sekta ya Elimu.
Mkutano huo ni wa nne kwa skuli binafsi, unaoitishwa kila mwaka na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Wizara na wadau wa skuli binafsi, kuboresha ubora wa elimu, pamoja na kutatua changamoto zinazojitokeza katika uendeshaji wa sekta ya elimu nchini.
Imetolewa na;
Kitengo cha Habari, Mawasiliano na Uhusiano - WEMA.

 

Post a Comment

0 Comments