Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi), Mhe. Hamza Hassan Juma, amewataka wafanyabiashara kuimarisha mahusiano mazuri ya kibiashara ili kuendeleza na kuitangaza Zanzibar kupitia maonesho ya biashara.
Mhe. Hamza ameyasema hayo Dimani, wakati wa hafla ya ufungaji wa Maonesho ya 12 ya Kimataifa ya Biashara ya Zanzibar, ambapo amesema Serikali itaendelea kuyaimarisha maonesho hayo ili yawe na tija zaidi katika kukuza sekta ya biashara na uchumi wa taifa.
Amesema maonesho ya biashara ni kielelezo cha kuyaenzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, kwani baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964, Wazanzibari waliamua kujikita katika kujikwamua kiuchumi kwa kujihusisha na ujasiriamali, biashara na kujiajiri.
Aidha, Mhe. Hamza amemshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa jitihada zake kubwa za kuinyanyua Zanzibar kimaendeleo kupitia maono yake ya kuijenga nchi kiuchumi na kijamii.
“Rais Dkt. Mwinyi anayatekeleza kwa vitendo maono ya Mwanzilishi wa Mapinduzi, Hayati Mzee Abeid Amani Karume. Amejenga shule za ghorofa, hospitali, nyumba za maendeleo na kutoa elimu bila malipo. Haya yote ni matunda ya Mapinduzi na mwendelezo wa nyayo alizopita Mzee Karume,” amesema Mhe. Hamza.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Dkt. Habiba Hassan Omar, amesema ushiriki mkubwa wa wafanyabiashara umefanikisha kwa kiasi kikubwa maonesho hayo na kuchangia kukuza maendeleo ya biashara nchini.
Amesema lengo la maonesho hayo ni kuwaunganisha wajasiriamali na wafanyabiashara ili kubadilishana mawazo, kupata mbinu mpya za ubunifu, masoko ya bidhaa, kuongeza uzoefu na kujifunza namna ya kunufaika na mitaji mbalimbali.
Dkt. Habiba ameeleza kuwa jumla ya washiriki 316 kutoka Zanzibar, Tanzania Bara na nchi za nje walishiriki katika maonesho hayo, wakihusisha sekta za umma na binafsi na kuonesha bidhaa na huduma mbalimbali.
Naye Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Zanzibar (ZCCIA), Amour Yussuf, amesema maonesho hayo ni jukwaa muhimu la kukutanisha wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi, kufungua fursa mpya za masoko na ushirikiano wa kibiashara.


0 Comments