ZANZIBAR – 4 FEBRUARI, 2026 –
Wakati timu yetu ya Wanasheria ikiwa mbele ya Mahakama Kuu kuomba Kukagua na Kupata nyaraka muhimu za uchaguzi (Application for Discovery and Inspection), Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kupitia Mwenyekiti wake, Jaji George Kazi, jana tarehe 3 Februari, 2026 imetangaza bila aibu mpango wa kuteketeza nyaraka zote zilizotumika katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa Oktoba 2025.
Haki Inacheleweshwa, Ushahidi Unateketezwa
Kwa muda wa wiki mbili sasa, tangu tarehe 21 Januari, 2026 maombi yetu ya kisheria ya kuiomba Mahkama itoe Amri kwa Tume ya Uchaguzi kuleta Mahkamani Nyaraka muhimu za uchaguzi kutokana na umuhimu wa nyaraka hizo katika kuamua Kesi zilizowasilishwa Mahkamani yamekwama katika Ofisi ya Msajili wa Mahakama Kuu bila sababu za msingi. Baada ya tangazo la jana, sasa tumefahamu kwamba kumbe kuchelewa huku si kwa bahati mbaya; ni mkakati wa makusudi wa "kupunguza kasi ya utafutaji haki" ili kuipa nafasi ZEC kuchoma ushahidi wa kile kilichotokea kwenye vituo vya kupigia na kuhesabu kura.
ZEC imeamua kujificha chini ya kifungu cha 98(3) cha Sheria ya Uchaguzi Namba 4 ya mwaka 2018 kinachohusu kutunza nyaraka kwa siku 90. Tuweke wazi: Ni kosa la Jinai kuharibu ushahidi wakati kuna shauri la kisheria linaloendelea. Kwa Tume ya Uchaguzi, ambayo yenyewe imetumia nyaraka hizo katika utetezi wake na inafahamu kwa uhakika kuwa nyaraka hizo kwa vyovyote iwavyo zitahitajika katika mashauri yaliopo Mahkamani ilipaswa ifahamu katika mazingira hayo kutumia kifungu kilichotajwa hapo juu ni kutumia Sheria kwa nia ovu na ni kuharibu Ushahidi kwa makusudi.
ZEC haiwezi kusema haifahamu jambo hili. Inalifahamu fika kwa sababu ni sehemu ya wadaiwa (respondents) kwenye mashauri yetu yaliyoko Mahakamani. Kuteketeza nyaraka hizi sasa siyo utaratibu wa kisheria—ni uhujumu wa ushahidi na dharau ya wazi kwa masuala yaliyoko Mahakamani. Kwa upande mwengine ni kufanya maamuzi kwa nia ovu (acting in bad faith) katika jambo linalohitaji kusimamia haki na uadilifu. Kama Tume ya Uchaguzi ingekuwa kweli makini wa kufuata Sheria kama inavyotaka watu waamini katika suala la kuteketeza nyaraka, leo tusingekuwa na mashauri ya kupinga Uchaguzi katika Majimbo 25 jambo ambalo ni rekodi ya kipekee tokea kufanyika kwa chaguzi Zanzibar kabla na baada ya Mapinduzi.
Lakini unapoyachukua mambo haya katika muktadha wake, ndipo unapogundua dhamira ovu na mchezo mchafu wa kusudio la kukanyaga haki za watu kwa mara ya pili – mara hii ikiwa ni kupitia ucheleweshaji wa haki na uteketezaji wa ushahidi – baada ya kwanza kuzikanyaga haki hizo kwenye vituo vya kupigia na kuhesabu kura.
Hapa ndipo mtu anapoelewa yanayoendelea - kwamba wakati Kanuni zinataka kesi zimalizwe ndani ya miezi 12, tayari miezi mitatu imepita bila ya kufika hatua yoyote ya maana Mahakamani. Kwa majimbo ya Unguja ndiyo kwanza usikilizwaji wa pingamizi unataka kusikilizwa mwezi wa pili mwishoni na mwezi wa tatu mwishoni wakati kesi zilifunguliwa (filed) tokea tarehe 5 Novemba, mwaka jana. Hali hii ni tofauti, kwa mfano, na Tanzania Bara ambapo Mahakama zimeshamaliza kusikiliza pingamizi za awali (POs) na sasa wapo kwenye kesi za msingi.
Kudharau Matakwa ya Wananchi
Hatua ya kutaka kuteketeza karatasi za kura, fomu za matokeo, na madaftari ya wapiga kura ni kukiri makosa kwa ZEC. Ikiwa uchaguzi ulikuwa huru na wa haki kama wanavyodai, kwa nini Tume iwe na haraka kiasi hiki kuchoma ushahidi? Haraka hii ya mara hii ya kutaka kuteketeza nyaraka za uchaguzi mara tu baada ya siku 90 haikuwahi kuonekana katika chaguzi zote sita zilizopita – kuanzia ule wa mwaka 1995 hadi ule wa mwaka 2020.
Isitoshe, katika majibu yao kwenye hati za kesi ya msingi (Reply to Petitions), ZEC wenyewe wameambatanisha fomu za majumuisho ya matokeo kwa kila kituo maarufu kama Fomu Na. 13B. Swali linakuja: Je, wanakwenda kuchoma moto ushahidi ambao wao wenyewe wameieleza Mahakama kuwa wanakusudia kuuleta Mahakamani?
Huwezi kuchoma eneo la tukio la uhalifu (crime scene) isipokuwa kama unajaribu kuficha jinai hiyo. Hiki ni kitendo cha kukata tamaa kwa taasisi inayoogopa ukweli na inayodharau akili za Wazanzibari.
Aibu, Fedheha na Kashfa
Tangazo la jana la Mwenyekiti wa ZEC ni la aibu, fedheha na kashfa. Ni kielelezo chengine cha ZEC kujivua nguo na kisha kujianika hadharani mbele ya Wazanzibari na Ulimwengu jinsi walivyoshindwa kuheshimu maadili ya kazi yao ambayo yanataka wasimamie haki na kuonesha uadilifu. Tume nzima ya Uchaguzi kuanzia Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wake ambao ni Majaji wa Mahakama Kuu, Makamishna wake wote pamoja na watendaji wa Tume wanapaswa wajitathmini.
Kitendo cha kutaka kuteketeza ushahidi huku kukiwa na kesi za kupinga matokeo ya uchaguzi Mahakamani ni kuwadharau Wazanzibari walio wengi. Tukumbuke kwamba kesi za kupinga matokeo ya uchaguzi kwa Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi zilizoko Mahakamani ni za majimbo 25 kati ya majimbo yote 50 ya Uchaguzi Unguja na Pemba. Hiyo ni asilimia 50 ya majimbo yote. Kwa maneno mengine, angalau nusu ya Wazanzibari wanahoji utendaji wa Tume hii jinsi ilivyoendesha Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Ni vyema pia ieleweke kwamba kesi hizi hazihusu haki za ACT Wazalendo; zinahusu haki za wananchi wa Zanzibar. Kutaka kuangamiza Ushahidi wa kesi hizi ni kuonesha jinsi ZEC inavyowadharau Wazanzibari ambao ilipaswa kuwalindia haki yao kuu ya kikatiba na kiraia, yaani haki ya kuchagua na kuchaguliwa – haki ya kuiweka madarakani Serikali wanayoitaka.
Kwa tangazo la jana, ZEC wamewadharau Wazanzibari kwa kudhani kuwa wakitaja kifungu cha sheria ndiyo watakuwa wamefunika dhamira yao ovu na mchezo wao mchafu na kwamba Wazanzibari hawana akili za kung’amua hilo.
Kwa hakika, dhamira ovu na mchezo mchafu huu ukitekelezwa unakwenda kuzinajisi Mahakama Zanzibar na pia kuhujumu hata hatua zinazoendelea zenye lengo la kutafuta ufumbuzi wa mkwamo uliopo ambao ulisababishwa na ZEC hiyo hiyo.
Tunapenda hapa kukumbusha kwamba Chama chetu kiliwasilisha Tume ya Uchaguzi barua afajiri ya tarehe 30 Oktoba 2025 [chini ya saa 24 tokea kura zikamilike kupigwa] kueleza kwa kina jinsi Uchaguzi ulivyovurugwa ikibainisha vitendo vyote vya kiharamia, vilivyofanywa na maofisa mbali mbali wa Serikali wengi wao wakiwa watumishi wa Tume ya Uchaguzi. Tume, kwa nia ovu ya wazi, haikutaka hata kuchunguza tuhuma hizo na kama kawaida yake ikaanza kujificha nyuma ya visingizio vya taratibu na Sheria.
Madai Yetu
Chama cha Act Wazalendo hakitakaa kimya wakati haki za wananchi wa Zanzibar na demokrasia yetu vikiendelea kuchanwa-chanwa na kutupwa kwenye moto. Hivyo, tunataka mambo yafuatayo yatekelezwe:
1. Kusimamishwa Mara Moja Uteketezaji: ZEC lazima isitishe mara moja mpango wowote wa kutupa au kuteketeza nyaraka na vifaa vya uchaguzi mpaka mashauri yote yaliyopo Mahakamani yamalizike.
2. Hatua za Haraka za Mahakama: Msajili wa Mahakama Kuu anapaswa ashughulikie maombi yetu ya ukaguzi wa nyaraka (Application for Discovery and Inspection) kwa haraka sana. Siku moja ya ukimya wa Mahakama ni ushirikiano katika kuharibu ushahidi.
3. Ulinzi wa Nyaraka na Vifaa: Tunatoa wito kwa mamlaka zote zinazohusika kuhakikisha kuwa nyaraka zote za Uchaguzi Mkuu wa 2025 zinatunzwa chini ya ulinzi madhubuti ili kuzuia "moto wa ajali" au upotevu.
Ukweli hauchomeki kwa moto.
ISMAIL JUSSA
MAKAMU MWENYEKITI (ZANZIBAR)
ACT WAZALENDO
.jpeg)

0 Comments