6/recent/ticker-posts

Jalsa ya Dua na Mafunzo Kwa ajili ya kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Riziki Pembe Juma, akizungumza katika kongamano la  Jalsa ya Dua na Mafunzo  Kwa ajili ya kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani iliyoandaliwa na Jumuiya ya Kuimarisha Taaluma na Maadili ya Kiislamu Zanzibar (JUKTAMKIZ) katika Skuli ya Sekondary ya  Haile Sallassie, Wilaya ya Mjini


Mwenyekiti wa Jumuiya ya kuimarisha  Taaluma na Maadili ya Kiislamu Zanzibar ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa AHSA, Ukhty Saada Mohamed Nassor, akielezea harakati za Jumuiya ya JUKTAMKIZ kwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Riziki Pembe Juma, katika Skuli ya Sekondary ya  Haile Sallassie, Wilaya ya Mjini.

Wanajumuiya ya kuimarisha Taaluma na Maadili ya Kiislamu Zanzibar wakimsikiliza Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Riziki Pembe Juma, katika Skuli ya Sekondary ya  Haile Sallassie, Wilaya ya Mjini

Wilaya ya Mjini, Zanzibar – 15/02/2026


Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Riziki Pembe Juma, amewahimiza waumini wa Kiislamu kuutumia Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kama fursa ya kujenga uhusiano mwema na Mwenyezi Mungu kwa kuongeza ibada, kuisoma Qur-an kwa wingi na kujipamba na tabia njema.

Akizungumza katika kongamano la  Jalsa ya Dua na Mafunzo  Kwa ajili ya kuukaribisha Mwezi Mtukifu wa Ramadhani iliyoandaliwa na Jumuiya ya Kuimarisha Taaluma na Maadili ya Kiislamu Zanzibar (JUKTAMKIZ) katika Skuli ya Sekondary ya  Haile Sallassie, Wilaya ya Mjini.

amesema Ramadhani si mwezi wa kufunga pekee, bali ni mwezi wa kusoma  Qur-an na kufuata mafundisho yake katika maisha ya kila siku.

Amesema ni wajibu wa kila muumini kujiandaa kiroho kwa kufanya ibada mbalimbali, kusaidiana kwa hali na mali, pamoja na kujiepusha na mambo yote yaliyokatazwa ili kufikia malengo ya Ramadhani.

Amewataka  wazazi na walezi, kuwa walimu wa kwanza wa watoto wao katika familia na wanapaswa kuwalea vijana katika misingi ya imani, maadili mema na kupenda ibada za usiku kama Tarawehe na Tahajjud ili kujenga jamii bora yenye hofu ya Mwenyezi  Mungu.

Akitoa Wito Kwa wafanyabiashara, amewasihi kuacha tabia ya kupandisha bei za bidhaa katika kipindi cha mwezi wa Ramadhani kwani kuwafanyia wepesi waumini ni sehemu ya kuchuma kheri na baraka za mwezi huo mtukufu.

Vilevile, amewahimiza wananchi kudumisha amani, umoja na mshikamano katika Taifa, akieleza kuwa bila ya amani hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana.

Hata hivyo  alimshukuru Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Ukhty Saada Mohamed Nassor, kwa kuandaa kongamano hilo kwa juhudi zake katika kuimarisha maadili ya vijana, Zanzibar.

 Amefahamisha kwamba  Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za dini katika kudumisha amani, maadili mema na mshikamano nchini.

Nae Mwenyekiti wa Jumuiya ya kuimarisha Taaluma na Maadili ya kiislamu Zanzibar (JUKTAMKIZ)  ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa AHSA, Ukhty Saada Mohamed Nassor, amesema kuwa lengo kuu la jumuiya hiyo ni kuimarisha maadili, elimu na ustawi wa jamii Zanzibar.

Amesema jumuiya hiyo imekuwa ikitoa elimu ya dini na maadili kwa jamii, kusaidia mayatima na watu wenye mahitaji maalum, kukuza vipaji vya vijana pamoja na kupambana na vitendo vya udhalilishaji na mmomonyoko wa maadili. Aidha, jumuiya hiyo imeweka mkazo katika kuwainua wanawake kiimani na kimaadili kwa kuzingatia misingi ya Kiislamu.

Ukhty Saada amefahamisha kuwa dira ya JUKTAMKIZ ni kujenga jamii inayofuata mwenendo wa Mtume Muhammad (SAW) katika maisha ya kila siku.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa juhudi zake za kuwasimamia na kuwaongoza wananchi kwa mapenzi makubwa, pamoja na kudhamini mchango unaotolewa na jumuiya hiyo katika maendeleo ya jamii.

Amesema mafanikio ya JUKTAMKIZ
 yametokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya jumuiya hiyo, Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar pamoja na Ofisi ya Msajili wa Jumuiya, ambapo wamekuwa wakitoa usimamizi, mwongozo na kuimarisha mshikamano wa kiserikali.

Akielezea historia ya jumuiya hiyo, amesema ilianzishwa kwa lengo la kuimarisha maadili ya Kiislamu kwa kushirikiana na taasisi za kidini na Serikali, na imekuwa ikitekeleza programu zake katika maeneo ya Unguja na Pemba kwa ufanisi.

Katika kongamano hilo  kulisomwa Dua na Nadwa katika kuukaribisha Mwezi wa Ramadhani, ikiwemo jinsi ya kuiandaa nafsi kabla ya Ramadhani ,nafasi ya Taraweeh,Witri na Qiyamullaylna laylatulqadir ,nafasi ya Qur'an pamoja na lishe na Ramadhani.


Imetolewa na Kitengo cha Habari .
WHSUM.

 

Post a Comment

0 Comments