
Mkoa wa Mjini Magharib .15-2-2026.Mwenyekiti wa ACT Taifa Mhe. Othman Masoud , amesema kwamba bila uchaguzi huru na wa haki kwenye taifa lolote watu wote watakuwa ni watumwa ndani ya nchi yao kwa sababu haki ya kwanza ya wananchi ni uwezo wa kuweka kiongozi unayemataka.
Mhe. Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar mstaafu ameyasema hayo ukumbi wa Majid Kiembesamaki mkoa wa mjini Magharib alipozungumza na viongozi wa chama hicho wa ngazi mbali mbali kutoka mikoa yote ya Unguja kutoa ufafanuzi kuhusia na maendeleo ya mazungunzo ya kisiasa yanayoendelea.
Amesema kwamba inapotokea mwananchi hana haki ya kuchagua na kuchaguliwa ni wazi kwamba hakuna tofauti na kuwepo kwa ukoloni ndani ya taifa lao jambo ambalo halipaswi kuwepo kwenye taifa lolote.
Aidha amesema pia unapokosekana haki ya namna hiyo katika taifa hilo hakutakuwa na uwajibikaji na madaraka yanapotumika vibaya hakuna wakuchunguza kiongozi na na kamwe taifa halitakuwa na mafanikio.
Mhe. Othman amesema kwamba iwapo serikali na viongozi hawachungzwi kisheria na kikatiba hakuna namna ya kuepuka wizi na ufisadi serikali na kuendelea kuwepo matumizi mabaya ya madara ya umma kwa waliopo serikalini waliopewa dhamana ya kusimamia mambo ya umma ndani ya taifa hilo.
Amesema kwamba harakati za chama chake cha ACT kinapambania kuondosha mfumo na utaratibu mbovu katika kusimamia na kuendesha nchi na pia kuondoa migogoro ambayo kwa baadhi ya watu ni mtaji wa kujinufaisha binafsi na wanakuwa ni wazito kuridhia inapotokea kuwepo makubaliano pale penye mgogoro.
Hivyo , amesema kwamba hakuna nchi inayoweza kusonga mbele na ikawa na utulivu na amani ya kweli na maendeleo thabiti kama nchi hiyo haina katiba bora na pia viongozi waliopo wakailinda na kuifuata kikamilifu misingi ya katiba waliyonayo.
Amefahamisha kwamba kuwepo mifumo bora na katiba yenye misingi madhubuti ndio inayosaidia kuwaweka wananchi pamoja na taifa likaweza kusonga mbele na kupata mafanikio ya kimaendeleo.
Mhe. Othman aliyekuwa akifafanua hoja za mazungunzo ya kutafuta muafaka wakisiasa yanayoendelea, amesisitiza kwamba msingi wa fitna iliyopo Zanzibar pamoja na mambo mengine ni kukosekana katiba bora na kuwepo mfumo mbaya wa uchaguzi ambapo anatokea mtu mmoja akamtangaza kiongozi kushinda uchaguzi pasipo na mamlaka ya kuhojiwa kwa kuwa katiba inatoa mamlaka ya kifalme kwa waliopo madarakani.
Amesema kwamba mazunguzo yanayoendelea ambayo yapo katika hatua kubwa ,chama chake kinahitaji kuwepo makubaliano yataweza kusaidia kuijenga msingi imara ya kikatiba Zanzibar , mfumo bora wa uchaguzi na kusimamia vyema haki za kidemokrasia na uwajibikaji kwa manufaa ya Zanzibar.
Amesema kwamba Zanzibar inahitaji kuwa na umoja wa kitaifa na maridhiano ya kweli kwa manufaa ya taifa na kwamba si vyema nchi ikaendelea hivi inavyokwenda sasa na kwamba ni vyema ikikubalika serikali ya pamoja isiwe ya paaa moja ikawanufaisha wachache kwa kupata vyeo.
Pamoja na hayo amesema kwamba ipo orodha ya mambo 12 muhimu ambayo yamejadiliwa ili na mengine yakikubalika yaweze kufanya kazi vizuri katika kuchapuza kasi ya kuleta mageuzi ya kweli Zanzibar, hata hivyo hakufafanua zaidi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho upande wa Zanzibar Ismali Jussu Ladhu, amewashukuru wanachama wote wa chama hicho kwa kuonesha na kufahamu dhamira ya kinachopambaniwa na chama hicho na kwamba wamekuwa wakijitolea kufanya shughuli zote za chama kwa ari kubwa jambo ambalo linakifanya chama hicho kuimarika licha ya misukosuko kinayopata.
Aidha amewataka wanachama kufanya kazi kwa pamoja katika kutimiza yale yote yaliyodhamiwa na kuweka malengo kuhakikisha kwamba chama kinatimiza azma yake ya kujenga na kumiliki ofisi na kumbi za mikutano za kimataifa.
Naye Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho Babu Juma Duni Haji, amesema kwamba viongozi wa Zanzibar kamwe hawapaswi kuyasahau malengo na dhamira ya mapinduzi ya mwaka 1964, kwamba ni ya kuondoa ubaguzi, mifarakano na dhulma za aina yoyote sambaba na kujenga maridhiano mingoni mwa wananchi wa Zanzibar.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar Omar Ali Shehe, amesema kwamba Viongozi wa chama hicho ngazi mbali mbali wameendelea kufanya kazi kila siku katika kuhakikisha kwamba chama kinaaimarika na licha ya misukosuko ya uchaguzi, lakini kimeendelea kuimarika kutokana na kazi kubwa ya kujenga chama inayoendelea kufanyika.
Amesema kwamba ahadi ya watendaji wa chama hicho ni kuhakikisha mbele ya mwenyekiti wa taifa kwamba hatua yoyote itakayofikiwa kwenye mazungunzo hayo wanachama wote wapo pamoja na viongozi na na kamwe hawatorudi nyuma kwa kuwa wanapigania haki.
Mhe. Othman amekamilisha vikao vyake na viongozi wa chama hicho ngazi mbali mbali Unguja na Pemba kuelezea juhudi za mazungunzo yakisiasa yanayoendelea pamoja na hatua iliyofikiwa yaliyoanza Novemba mwaka jana mara baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, ambapo tume ya uchaguzi Zanzibar ilimtangaza Dk. Mwinyi kuwa mshindi jambo lililopigwa na ACT kwa madai kwamba uchaguzi uligubigwa na hila , wizi wa kura na udanganyifu.
Mwisho.
Imetolewa na Ofisi ya Mwenyekiti wa Taifa wa ACT leo Jumapili Februari 15, 2026.


0 Comments