6/recent/ticker-posts

Jamii Yatakiwa Kujenga Tamaduni ya kupima afya Mara kwa Mara

Na.Mwandishi Wizara ya Afya Zanzibar. 

Jamii imetakiwa kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara ili kubaini dalili za awali za ugonjwa wa saratani na kuanza matibabu mapema kabla ugonjwa huo haujafikia hatua hatarishi.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Maradhi Yasiyoambukiza Zanzibar, Dkt. Omar Mohamed Suleiman, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Saratani Duniani, ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 4 Februari.

Dkt. Suleiman amesema kuwa katika kipindi cha takribani miaka mitano, wagonjwa 1,533 wa saratani wamepokelewa katika huduma za oncology, ambapo zaidi ya vifo 400 vimeripotiwa. Ameeleza kuwa saratani zinazoongoza ni pamoja na saratani ya matiti, ubongo, mlango wa kizazi na tezi dume.

Ameongeza kuwa sababu nyingi zinazosababisha saratani zinaweza kuzuilika, zikiwemo matumizi ya tumbaku, lishe duni, kutofanya mazoezi, unene uliopitiliza, matumizi mabaya ya pombe, pamoja na maambukizi ya virusi vya HPV na Hepatitis B na C.

Kwa upande wake, Harrieth Hamis kutoka shirika la Jhpiego amesema kuwa wanaume wamekuwa wagumu kujitokeza kupima saratani ya matiti kutokana na dhana potofu kwamba ugonjwa huo huwapata wanawake pekee, jambo ambalo si sahihi.

Amefafanua kuwa saratani ya matiti huwapata watu wa jinsia zote, hivyo ni muhimu kwa wanaume kujitokeza wakati wa huduma za mkoba zinazotolewa katika jamii ili waweze kujitambua mapema na kuanza matibabu kwa wakati.

Ameongeza kuwa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Pfizer Foundation na shirika la Jhpiego, ndani ya kipindi cha miaka miwili iliyopita, imefanikiwa kuwachunguza wanawake 14,000, ambapo asilimia 7 walibainika kuwa na matatizo mbalimbali, ikiwemo watu 72 waliothibitika kuugua saratani ya matiti.

Post a Comment

0 Comments