6/recent/ticker-posts

Katibu Mkuu Kiongozi ahimiza ushirikiano Wizara ya Afya




Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said, amesema ushirikiano wa Wizara ya Afya, taasisi za Serikali, sekta binafsi pamoja na wadau wa maendeleo ni nguzo muhimu katika jitihada za kutokomeza ugonjwa wa malaria Zanzibar.
Amesema hayo wakati akifungua mkutano wa Makatibu Wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar uliofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege, mkutano uliolenga kuzishirikisha sekta zisizo za afya katika mapambano ya kumaliza malaria.
Mhandisi Zena amesema Zanzibar imefanikiwa kupunguza maambukizi ya malaria hadi kufikia asilimia moja kutokana na juhudi za Serikali, lakini amesisitiza kuwa lengo ni kufikia asilimia sifuri. Hivyo amezitaka taasisi za Serikali na binafsi kuongeza ushirikiano ili kufikia lengo hilo.
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Dk. Islam Seif Salum, amesema ugonjwa wa malaria unaathiri sekta ya utalii na uchumi wa Zanzibar kwa ujumla, na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Naye Meneja wa Programu ya Maliza Malaria Zanzibar (MEZA), Richard Silumbe, amesema mradi huo unalenga kuifanya Zanzibar kuwa salama na huru dhidi ya malaria kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. Mngereza Mzee Miraji, amesema ushirikiano wa sekta mbalimbali utaongeza ufanisi wa juhudi za Serikali katika kutokomeza malaria Zanzibar.


 

Post a Comment

0 Comments