Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua hatua thabiti ya kuweka mazingira bora ya kufanyia kazi kwa Mhimili wa Mahakama.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussein Ali Mwinyi katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya sheria Zanzibar yaliyofanyika katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete Pemba.
Amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali imewekeza zaidi ya fedha za Kitanzania shilingi bilioni 13.6 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya kisasa ya Mahakama ambayo yanaendana na uwekaji wa miundombinu ya Tehama pamoja na upatikanaji wa vitendea kazi.
Aidha, Mhe. Hemed amefahamisha kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika matumizi ya Tehama kuelekea Serikali Mtandao, ili kutimiza azma ya kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali hasa katika matumizi ya mfumo wa usimamizi wa mashauri pamoja na mifumo mengine itakayozidisha uwajibikaji katika mchakato mzima wa upatikanaji wa haki.
Amesema kupitia mfumo huo usajili wa mashauri utakuwa rafiki, usikilizaji na uamuzi wa mashauri utafanyika kwa haraka sambamba na upatikanaji sahihi wa takwimu, kuongezeka kwa uwazi na kukuza uwajibikaji miongoni mwa wadau wa Sheria.
Hata hivyo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameupongeza Uongozi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar kwa kuifanyia kazi sheria ya Mwenendo wa wa Madai ya Zanzibar (Civil Procedure Decree Chapter 8) ya mwaka 1917 ambapo rasimu ya sheria mpya na kanuni kadhaa zimeshatayarishwa.
Amewakumbusha watendaji wa Mahkama kwamba sheria umuhimu wa sheria hio na ndio inayobeba mustakbali wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kusema kuwa ustawi wa biashara na uwekezaji unategemea ubora wa sheria hio.
Akitoa salamu za Mahkama Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla amesema Matumizi ya Tehama yataleta mageuzi makubwa ya kiutendaji kwa kufanya kazi kwa ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika kufikia upatikanaji wa haki kwa wananchi.
Jaji Ramadhan amesema mifumo mitano imeundwa kwa ajili ya kurahisisha utendaji kazi wa mahkama ikiwemo mfumo wa usimamizi wa mashauri ambao utazifanya mahkama kuondokana na matumizi ya makaratasi na mawakili watafungua mashauri ya kesi bila ya kufika mahakamani.
Aidha, amefahamisha kuwa mafunzo ya utumiaji wa mifumo hio yanaendelea kutolewa kwa watumishi na wadau wa Sheria Unguja na Pemba mafunzo ambayo yataleta mageuzi makubwa katika utowaji wa huduma za kimahkama Zanzibar.
Jaji Ramadhan ameitaja mifumo inayotumiwa na Mahkama za Zanzibar kuwa ni pamoja na mfumo wa usimamizi wa mashauri, Mfumo wa ZAN-WAKILI, Mfumo wa Tume ya Utumishi ya Mahakama, Mfumo wa Malalamiko na utowaji wa maoni pamoja na Mfumo wa Uhifadhi wa hukumu za Mahakama.
Nae Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Mwalim Dkt. Haroun Ali Suleiman amesema Wizara yake itaendelea kushirikiana na watendaji wa Mahkama katika kuhakikisha wanafanya kazi katika mazingira bora, wezeshi na salama hasa kutokana na usiri wa utendaji kazi wa Muhimili huo.
Dkt. Haroun amezipongeza Taasisi zote zinazosimamia Sheria kwa uwajibikaji wao, kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano hasa katika kusimamia upatikanaji wa haki kwa wananchi.
Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar Mhe. Mgeni Jailani Jecha amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuboreshwa mifumo ya Mahkama ili kuendana na kasi ya utendaji wa kazi kwa haki na uwazi.
Mhe. Jailani amesisitiza kuwa uwepo wa Mifumo ya Teknolojia kwa Mahakama za Zanzibar kutatahisisha uwendeshaji wa kesi kwa uharaka na uwazi, kupunguza changamoto ya mashahidi kutokufika Mahkamani lakini pia kuwaweka mashahidi katika hali ya usalama,uhuru na kujiamini katika utowaji wa ushahidi .
Amesema utaratibu wa utunzaji wa kumbukumbu sio nzuri na salama kwa Mahkama za nzibar hivyo ujio wa matumizi ta Tehama utawezesha utunzaji wa kumbukumbu za mwenendo wa kesi kwa ajili ya ukataji wa rufaa na mahitaji mengine muhimu ya kimahkama.
Kwa upande wake raisi wa Chama cha Mawakili Zanzibar Mhe. Joseph Magazi amesema utowaji wa haki unahitaji kuendana na matumizi ya Tehama katika upatikanaji wa haki, kurahisisha ufikiwaji wa elimu ya sheria sambamba na kupanua wigo wa ufahamu wa sheria kwa wananchi waliowengi.
Mhe. Magazi amefahamisha kuwa katika kuunga mkono matumizi ya Tehama Chama cha Mawakili Zanzibar kitaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na elimu ya matumizi ya Mifumo katika upatikanaji wa haki jinai, uwazi wa uendeshwaji wa kesi na utowaji wa ushahidi kwa mashahidi popote walipo.
Imetolewa na kitengo cha Habari ( OMPR )
Leo tarehe 09 / 02 / 2026
%20(1).jpeg)
%20(1).jpeg)
%20(1).jpeg)
%20(1).jpeg)
0 Comments