Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Mahmoud Mussa Wadi amewataka Wauguzi na wakunga nchini kuzingatia maadili, huruma na misingi ya imani za dini kama nguzo muhimu katika utoaji wa huduma za afya, amewakumbushwa kuwa taaluma yao si ajira tu bali ni dhamana, ibada na sadaka mbele ya Mwenyezi Mungu.
Wito huo ameutoa wakati wa uzinduzi wa semina elekezi kwa wasimamizi wa wauguzi na wakunga kuhusu maadili na huduma stahiki kwa mujibu wa imani za dini, uliofanyika katika ofisi za Wizara ya Afya, Mombasa.
Alibainisha kuwa kila huduma ya afya inayotolewa kwa huruma, ujuzi na weledi ni ibada mbele ya Allah (s.w), na kwamba Mwenyezi Mungu ameahidi malipo kwa wale wanaotekeleza majukumu yao kwa ikhlasi.
Alionya dhidi ya uzembe, hususan katika nyakati za dharura, akisisitiza kuwa kuacha mgonjwa mahututi bila huduma ni kinyume na maadili ya dini na taaluma.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Mngereza Mzee Miraji, alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika miundombinu na vifaa tiba ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya.
Alionya kuwa jitihada hizo zitakuwa bure endapo wahudumu wa afya, hususan wauguzi, hawatafanya kazi kwa imani, kujituma na kujitoa.
Dkt. Mngereza alisema dhamana ya afya za Wazanzibari iko mikononi mwa wauguzi kutokana na dhamana waliyoibeba mbele ya Mwenyezi Mungu, akisisitiza kuwa Serikali ikishatekeleza wajibu wake, kilichobaki ni wahudumu kusimamia viapo vyao vya kazi kwa uadilifu.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Ukunga na Uuguzi, Mwanaisha Fakih, alisema kada ya uuguzi imekuwa ikilalamikiwa mara kwa mara, jambo lililosababisha kuandaliwa kwa semina hiyo ili kuwajenga wauguzi na wakunga kwa misingi ya imani za dini na kubadili mitazamo hasi. Alisema semina hiyo itakuwa endelevu na itafanyika katika maeneo yote yanayotekeleza huduma za uuguzi.
Akiwasilisha mada katika semina hiyo, Mwakilishi kutoka Ofisi ya Mufti, Sheikh Shaaban Battash, ambaye pia ni mjumbe wa Baraza la Ulamaa na Mkuu wa Idara ya Utatuzi wa Migogoro, alisema uhai ni rasilimali kubwa na ya thamani kwa kila kiumbe, na kwamba wauguzi na wakunga ni sehemu ya kusimamia uhai au umauti wa watu.




0 Comments