6/recent/ticker-posts

Serikali yafanikiwa kwa kiwango kikubwa kuondoa uingiaji wa mikondo miwili kwa wanafunzi






SERIKALI imesema kwa kiasi kikubwa imefanikiwa kuondoa uingiaji wa mikondo miwili kwa wanafunzi wa sekondari na msingi kwa skuli za serikali Zanzibar.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar (WEMA) Mhe. Mhe. Lela Muhamed Mussa, aliyasema hayo katika kikao cha Waandishi wa Habari akieleza mafanikio ya sekta ya elimu, huko ofisi za wizara hiyo Mazizini, Mjini Unguja.

Alisema tayari asilimia 81 ya skuli za sekondari zinaingia mkondo mmoja, na asilimia 70 skuli za msingi zinaingia mkondo mmoja, na muda mfupi ujao wamejipanga kufikia asilimia 100 kwa wanafunzi hao.

Aidha alisema wanafunzi hao wamefikia 277 kwa ngazi ya sekondari, 341 ngazi ya msingi na 263 kwa maandalizi jambo ambalo linatokana na juhudi za makusudi zinazofanywa na serikali katika kuekeza kwenye majengo, kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.

Alieleza kuwa serikali inaendelea kutekeleza adhma yake ya kufanya mageuzi ndani ya sekta ya elimu kwa kuchukua jitihada mbalimbali ikiwemo kuajiri walimu 1,800, ujenzi wa miundo mbinu, mageuzi ya mtaala mpya na mabadiliko ya sera na sheria.

Akizungumzia vipaumbele vya wizara hiyo katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 alisema serikali imejipanga na ujenzi wa madarasa 1,008  dahalia 16, jengo la ukumbi wa mikutano utakao chukua watu 1,500 huko Taasisi ya sayansi na Teknolojia Karume.

Vipaumbele vyengine ni kuendeleza ujenzi wa wa Kampas ya kudumu ya Chuo Cha Teknolojia cha India Zanzibar (IITM) utanuzi wa Chuo Cha SUZA, pamoja na taasisi 74 kupangwa kuunganishwa na mkonga wa taifa.

Pia serikali imepanga kununua vifaa vya kisasa kwa ajili ya Smart classroom 25, Interactive Classroom 2,STEM Lab 2 na AI Computa Lab 2, laptop 4000 kwa wanafunzi, desktop 2,000 kwa maabara desktop 5000 kwa walimu wakuu wa skuli za serikali na smart Blackboadrs 25 ili kuimarisha ufundishaji kidigitali.

Pamoja na mambo hayo alisema jitihada za serikali zinaendelea katika kuanzisha vyuo vitakavyosimamiwa kisekta ili kujenga umahiri kwa wanafunzi wa ngazi ya cheti na Stashahada kwenye taasisi mbali mbali ikiwemo Afya, kilimo, Fedha na taasisi ya Kiswahili Mkurumah.

Akizungumzia matumizi ya mtaala mpya alisema tayari yameanza kwenye madarasa 40 ambapo mtaaña huo unahusisha utoaji wa fani mbali mbali kwa wanafunzi ikiwemo ushonaji na ufundi seremala.

Sambamba na hayo alifahamisha kuwa kwa kutambua umuhimu wa sayansi na teknolojia nchini serikali imeamua kujenga maabara maabara kuanzia ngazi ya skuli za msingi ili kuwawezesha watoto kukua na kupenda masomo ya sayansi kama ilivyo la lengo la serikali katika kukuza ufaulu wa masomo hayo.

Imetolewa na:

Kitengo cha Habari na Uhusiano (WEMA)


 

Post a Comment

0 Comments