6/recent/ticker-posts

Polisi Mkoa wa Songwe wakamata mmoja tukio la uporaji na kukamata gari lililoibiwa


 TAARIFA KWA UMMA

 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limefanikiwa kulikamata gari lililoibiwa aina ya Mitsubishi Outlander pamoja na mtuhumiwa mmoja, ambaye alikutwa akiwa na bastola ya kutengeneza kienyeji, baada ya kufanya msako mkali wa kuwatafuta watuhumiwa hao.

 

Tukio hilo linahusiana na wizi wa gari uliotokea tarehe 16/12/2025 saa 06:00 usiku, katika Mtaa wa Uwanjani, Tarafa ya Tunduma, Wilaya ya Momba, Mkoa wa Songwe. Gari hilo aina ya Mitsubishi Outlander lenye namba za usajili T.897 EAC, chasis namba CW5W0008014 na engine namba 4B12AA5184, lenye thamani ya Shilingi 20,000,000/=, ni mali ya Jovin Kafana (37), mfanyabiashara (Agent) mkazi wa Tazara, Mji wa Tunduma Wilaya ya Momba Mkoani Songwe.

 

Gari hilo liliibiwa baada ya kuvamiwa na majambazi waliomtishia mmiliki kwa kutumia bastola hiyo ya kutengeneza kienyeji, na baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilianza mara moja jitihada za kuwatafuta watuhumiwa hao.

 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe liliendelea na msako mkali, na tarehe 06/02/2026 saa 17:30 jioni, askari wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe walipata taarifa za kiintelijensia kuwa gari hilo lipo Makambako Mkoa wa Njombe. Walipofika Makambako, walimkamata mtuhumiwa aitwaye Bashiru Madembwe (35), fundi magari wa Mkazi wa Makambako Mkoa wa Njombe, ambaye aliwapeleka askari kuwaonesha gari hilo alipolificha katika Kitongoji cha Ipilimo Kijiji Cha Iyai,  Kata Ya Ihowanza, Tarafa Ya Malangali, Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa.

 

Vilevile, Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limefanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja (jina lake limehifadhiwa kwa ajili ya upelelezi) aliyehusika katika tukio la unyang’anyi wa kutumia silaha lililotokea tarehe 04 Februari, 2026 saa 04:00 asubuhi, katika eneo la Kisimani, Mtaa wa Unyamwanga, Kata ya Tunduma, Wilaya ya Momba, Mkoa wa Songwe.

 

Katika tukio hilo, mtuhumiwa huyo na wenzake walimfyatulia risasi Yengo Mwapina, mkazi wa Sogea, Wilaya ya Momba, Mkoa wa Songwe, na kumsababishia jeraha katika kiuno upande wa kushoto, pamoja na kumnyang’anya fedha kiasi cha Shilingi Milioni Hamsini na Nne za Kitanzania (54,000,000/=) akiwa anatokea benki ya NBC Tunduma.

 

Watuhumiwa hao bado wanashikiliwa kwa ajili ya mahojiano ili kubaini mtandao wao na watu wengine wanaoshirikiana nao katika vitendo vya ujambazi na unyang’anyi kwa kutumia silaha katika maeneo mbalimbali ya Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, na baada ya kukamilika kwa mahojiano hayo, hatua za kisheria zitaendelea kuchukuliwa dhidi yao.

 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linatoa onyo kali kwa watu wote wanaojihusisha na vitendo vya ujambazi, unyang’anyi kwa kutumia silaha na uhalifu wa aina yoyote kuwa hakuna mahali pa kujificha, kwani lina mtandao mpana wa kiintelijensia na linaendelea kufanya operesheni kali, ambazo ni endelevu na zisizotabirika pia linawaonya wahalifu wote kuwa mkono wa sheria ni mrefu, na yeyote atakayejihusisha na vitendo hivyo atakamatwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, vilevile linaendelea kuwaomba wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwani usalama ni jukumu la kila mmoja wetu.

 

Imetolewa na:

Kamanda wa Polisi,

Mkoa wa Songwe.

Post a Comment

0 Comments