Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na washiriki wa maadhimisho ya kutimia miaka kumi (10) kwa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki yaliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja, Zanzibar.
Serikali zote mbili zinatambua na kuthamini kazi kubwa na nzuri zinazofanywa na Kamisheni ya ya Lugha ya Kiswahili ya Afrika Mashariki katika kuikuza na kuiendeleza lugha ya kiswahili katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla katika hafla ya Maadhimisho ya Miaka 10 ya Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki yaliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar.
Amesema Jitihada kubwa zimechukuliwa na Kamisheni ya lugha ya kiswahili Afrika mashariki ikiwemo kuhakikisha wanajumuia ya Afrika Mashariki wanatumia lugha ya kiswahili katika mawasiliano yao ya kila siku jambo linalopelekea kuzidi kukua na kusambaa kwa haraka kwa lugha hio.
Mhe. Hemed amefahamisha kuwa kutokana na ukubwa wa lugha ya kiswahili ni jukumu la Kanisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki kuzihamasisha nchi wanachama kuanzisha mabaraza yatakayoratibu shughuli za matumizi na maendeleo ya kiswahili ili kuweza kufikia maendeleo endelevu ya Jumuiya hio.
Aidha, Mhe. Hemed amesema hatua iliyochukuliwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO ) ya kuiweka lugha ya kiswahili kuwa ni lugha ya kazi katika Shirika hilo inaongeza fursa ya kufungua milango ya lugha hio kwa wataalamu wa kiswahili ambapo ameitaka Kamisheni hio kujipanga katika kuzitumia vyema fursa hizo na kuhakikisha wanachama wote wananufaika na fursa hizo.
Sambambana hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameihakikishia Kamisheni ya lugha ya Kiswahili ya Afrika Mashariki kuwa Serikali zitaendelea kutoa kila aina ya ushirikiano ili kuhakikisha lugha ya kiswahili inapata maendeleo makubwa na kuwanufaisha wataalamu na wananchi zote.
Mhe. Hemed ameitaka Kamisheni hio kuongeza juhudi na ubunifu ili kuhakikisha malengo na mafanikio katika Kamisheni na jumuiya za kiswahili yanakuwa endelevu na yenye kuleta tuja katika maendeleo ya lugha ya Kiswahili.
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Mhe. Dkt. RIZIKI PEMBE JUMA ameipongeza Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki kwa kutimiza miaka kumi ( 10 ) ambayo imetanua wigo mpana katika kuiletea lugha ya kiswahili maendeleo makubwa hasa katika kuratibu na kuineza lugha ya hio kwa ufasaaha zaidi.
Mhe. Dkt. Pembe amesema KAKAMA inaendelea kuimarisha ustawi wa kiswahili Afrika Mashariki na kuwa kiungo muhimu cha mawasiliano ya kikanda na Kimataifa.
Amewataka nchi wanachama wa Jumiya ya Afrika mashariki kwa kushirikiana na KAKAMA kuhakikisha wanatumia nafasi ya utamaduni kwa kuieneza lugha ya kiswahili na kuwa daraja ka kufikia malengo ya kusambaa zaidi kwa lugha ya kiswahili.
Nae Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Jumuia ya Afrika Mashariki Mhe. BEATRICE ASKULI amesema kuanzishwa kwa Kamisheni ya Kiswahili Afrika Mashariki ni dhamira ya kweli ya kuziunganisha nchi za Afrika Mashariki ambapo lugha ya kiswahili imekuwa kiunganishi muhimu sana cha kuwaleta watu pamoja katika harakati mbali mbali za kimaendeleo.
Mhe. BEATRICE amezitaka nchi wanachana na wadau wote wa Kiswahili kuongeza juhudikatika kukiendeleza kiswahili na kuzitaka nchi ambazo hazina mabaraza ya kiswahili ya Taifa kufanya haraka kuanzisha mabaraza hayo ili kazi ya kukikuza na kukieneza kiswahili iweze kufikia malengo yake.
Akitoa salamu za mabaraza na wadau wa Kiswahili, Katibu Mtendaji Baraza la Kiswahili Taifa (BAKITA) Bibi CONSOLATA MUSHI amesema Kamisheni ya Kiswahili Afrika Mashariki inatimiza miaka 10 ikiwa imehakikisha lugha ya kiswahili imekuzwa, Imeimarika na kuenezwa vyema Barani Afrika na duniani kote.
Bibi CONSOLATA ameeleza kuwa KAKAMA imekipa hadhi kiswahili na kukifanya kuwa lugha rasmi ya mawasiliano, elimu na biashara pamoja na kuifanya kugha hio kuwa lugha ya kimkakati katika shughuli mbali mbali za maendeleo Nchini.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amekagua kazi za taasisi zinazojishuhulisha usambazaji wa lugha ya Kiswahili ndani ya jumuiya ya Afrika Mashariki.
Imetolewa na kitengo cha Habari ( OMPR )
Leo tarehe… 14 / 02 / 2026
0 Comments