6/recent/ticker-posts

OMO ahitimisha ziara kuwatembelea na kuwafariji Wananchi wanyonge





Mwenyekiti wa Taifa wa ACT Wazalendo, Mheshimiwa Othman Masoud Othman amesisitiza haja ya Viongozi kuwatembelea na kuwafariji Wananchi wanyonge, sambamba na kuziombea mafanikio juhudi za kuleta Maridhiano ya Kisiasa Zanzibar, zinazoendelea kati ya Upande wake na Chama Cha Mapinduzi (CCM) hasa ndani ya Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan.
Mheshimiwa Othman ameeleza haja hiyo leo Alhamis Februari 26, 2026, akiwasalimia Wananchi wa Mkoa wa Kichama wa Mjini Unguja, kwa nyakati tofauti, alipoendelea kuwatembelea na kuwajulia-hali Wazee, Wagonjwa na pia Watu wanaokabiliwa na matatizo mbali mbali ya kijamii wakiwemo Wafiwa na Wasiojiweza.
Amesema, kwa-mujibu wa taarifa za hivi punde amearifiwa na 'upande wa pili' kuwa wameketi kujadili juhudi za kuleta Maridhiano ya Kisiasa Nchini, na 'wamefikia pema', bali la muhimu zaidi ni kwa kila mmoja kuzidisha Dua, ili kuombea Mustakabali Mwema wa Mazungumzo yanayoendelea baina ya Vyama hivyo Vikuu vya Kisiasa, na Taifa kwa ujumla.
"Muhimu Nchi yetu irudi katika mstari wake; kama mnavyoona hali hivi ilivyo sasa, mambo hayaendi, au mnaonaje ndugu zangu", ameeleza na kuhoji Mheshimiwa Othman, huku akisisitiza haja ya kuendeleza Dua, Umoja na Mshikamano, hasa ndani ya Mwezi huu wa Kheri na Baraka.
Mheshimiwa Othman ameendelea kuzungumzia Ziara zake hizo kuwa ni Mwenendo Mwema ambao yeye na wenzake wameurithi kutoka kwa Wazee na hasa Mtangulizi wa Nafasi yake, Almarhum Maalim Seif Sharif Hamad.
"Tumeona hali ngumu za maisha zinazowakabili wananchi wetu; nami niwaombe Viongozi wote, kila mmoja kwa nafasi yake na mwenye uwezo, aweze kujitoa na kuwafikia Wananchi wetu wanyonge; twendeni tukawashike-mkono jamani kwa lengo la kuwasaidia ili kila mmoja angalau aifunge Ramadhani akiwa na furaha", amesisitiza Mheshimiwa Othman.
Akitoa salamu za shukran kwa niaba ya Wananchi wote, pamoja na Viongozi waliohusika na Ziara hiyo, Mwenyekiti wa Mkoa wa Kichama wa Mjini Unguja, Ndugu Haji Dude, ameshukuru kwa kile alichokitaja juhudi binafsi, hikma na hisia, ambazo Mheshimiwa Othman amezionyesha mbele ya Umma, licha ya hali na mazingira magumu yaliyopo sasa, kwa kuwafikia na kuwapa faraja takriban Wananchi Thelathini na Nne (34) kwa upande wa Unguja pekee, tangu ulipoingia Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, hatua ambayo amesema imeleta matumaini makubwa ya wananchi kwake.
"Kwa kweli, kutokana na juhudi na wema wako huu Mheshimiwa, tumefikia pahala ambapo Wazanzibari na Wananchi wote tumekuwa na matumaini nawe", amesema,
katika Ziara hiyo Mheshimiwa Othman, amewajulia-hali Bi. Fatma Choum Mdachi, Bw. Nassor Amour Ali, Bw. Khamis Othman Kondo, Bi Asha Mselem Hija, Bw. Makame Sharif Kombo, Bw. Nassor Mbarouk Juma, Bi Sharifa Hamad Salim, Bw. Abdalla Sheikhan Hussein na Bw. Suleiman Juma Khamis, wote wakaazi wa Mbuyuni-Basra, Amani Fresh, Shaurimoyo Mgandini, Sebleni, Magomeni-Gengeni, Migombani, Jang'ombe Msikiti wa Jeshi, Kisiwandui Msikiti-Makuti na Mji-Mkongwe 'Jaws Corner', katika Majimbo ya Chumbuni, Amani, Shaurimoyo, Kwahani, Magomeni, Mpendae, Jang'ombe, Kikwajuni na Malindi.
Ziara hiyo imewajumuisha pia Viongozi na Watendaji Wakuu wa Kichama wa Majimbo na wa Mkoa huo, wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho upande wa Zanzibar Ndugu Omar Ali Shehe na Naibu Katibu wao wa Haki za Binaadamu, Bi Pavu Abdalla Juma.
Mheshimiwa Othman amekamilisha Hatua hiyo kwa upande wa Unguja, ambapo anatarajiwa kuanza Ziara kisiwani Pemba, mwanzoni mwa Wiki ijayo.
Kitengo cha Habari
Ofisi ya Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Taifa
Februari 26, 2026.


 

Post a Comment

0 Comments