Kampuni ya Orbit Microfinance Limited imekabidhi vifaa mbalimbali vya elimu kwa wanafunzi wa Skuli ya Msingi na Maandalizi Kwarara, hatua inayolenga kuimarisha mazingira ya kujifunza na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya elimu.
Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na madaftari, kalamu na kampasi, ambavyo vitawanufaisha jumla ya wanafunzi 300, huku kipaumbele kikitolewa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum na wale wanaotoka katika mazingira magumu, ili kuhakikisha wanapata fursa sawa ya elimu.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo, Mkurugenzi wa Ustawi wa Jamii na Wazee, Maalim Hassan Ibrahim Suleiman, aliwataka wanafunzi hao kutumia vyema msaada walioupata kwa kusoma kwa bidii na kuzingatia nidhamu ili kufikia ndoto zao.
“Elimu ni ufunguo wa maisha. Msipoteze nafasi hii, someni kwa bidii ili muweze kutimiza malengo yenu na kuwa raia wema wa taifa,” alisisitiza Maalim Hassan.
Aidha, aliwahimiza wanafunzi kujifunza kutoa taarifa za vitendo vya udhalilishaji na ukatili kwa watu wazima wanaowaamini, ili kulinda usalama na ustawi wao.
“Mjifunze kusema hapana, sitaki. Msikubali kuingia kwenye mitego ya watu wanaofanya vitendo vya udhalilishaji,” aliongeza.
Pia aliwataka wanafunzi kuchagua marafiki wazuri wanaowajenga kimaadili na kitaaluma. Kwa upande mwingine, aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha huduma za elimu mijini na vijijini, huku akizitaka taasisi binafsi na wadau wa maendeleo kuiga mfano wa Orbit Microfinance kwa kutoa mrejesho kwa jamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Orbit Microfinance Limited, James Charles Challe, alisema taasisi hiyo inaamini kuwa elimu ni nyenzo muhimu ya maendeleo ya binadamu na msingi wa maendeleo endelevu ya taifa.
“Tunaamini kuwa uwekezaji katika elimu ni uwekezaji wa moja kwa moja katika mustakabali wa taifa. Vifaa hivi vitawasaidia wanafunzi kusoma kwa bidii na kufikia ndoto zao,” alisema Challe.
Aliwataka wanafunzi kuvitunza na kuvitumia vizuri vifaa hivyo, huku akiwapongeza walimu na wazazi kwa mchango wao mkubwa katika malezi na elimu ya watoto, akibainisha kuwa taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na jamii katika kuboresha ustawi wao.


0 Comments