Na.Omar Abdalla -Wizara ya Afya Zanzibar.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya imesema
itaendelea kushirikiana na washirika wa maendeleo wa sekta ya afya wakiwemo CDC
na Amref katika kuimarisha huduma mbali mbali Afya pamoja na Methadone (MAT) kwa
waathirika wa dawa za kulevya.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya
Zanzibar, Dkt. Mngereza Mzee Miraji, aliishukuru Amref Health Africa Tanzania
na (CDC) Tanzania kwa mchango wao mkubwa wa kuimarisha huduma za afya, hususan
kwa makundi yaliyo katika hatari zaidi.
Aidha Dkt Mngereza alieleza kuwa licha ya Zanzibar kuwa na
kiwango cha maambukizi ya VVU kilicho chini ya asilimia moja kwa idadi ya watu
kwa ujumla, bado kuna changamoto kubwa kwa watu wanaotumia dawa za kulevya kwa
njia ya sindano, ambapo maambukizi yanafikia asilimia 9.3. Alisisitiza kuwa
huduma za MAT zimekuwa nyenzo muhimu ya kupunguza madhara, kuzuia maambukizi
mapya ya VVU, na kuimarisha afya na maisha ya wananchi.
Amesema kwa kipindi cha miaka kumi CDC na Amref Afrika
wameshirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya
katika kuhakikisha kuwa maisha zaidi ya familia 1800 wamepatiwa huduma na kati
hayo mia tatu wanaendelea na maisha yao ya kawaida.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa wa Amref Tanzania, Dkt.
Florence Temu, amesema kuwa kupitia ushirikiano kati ya Amref Tanzania na CDC
Tanzania, jumla ya watu 1,831 (wanaume 1,745 na wanawake 86) wamefikiwa na
huduma za OAT/MAT hadi kufikia Desemba 2025.
Amefahamisha kuwa huduma hizo zimejumuisha upimaji na
matibabu ya VVU, uchunguzi na tiba ya kifua kikuu, huduma za homa ya ini
(hepatitis), pamoja na ushauri nasaha na elimu ya afya.
Aliongeza kwa kusema jumla ya wahudumu 21 wa afya na
waelimishaji rika wamepatiwa mafunzo ya kitaalamu, huku watumishi watatu
waliokuwa chini ya mradi wanatarajiwa kuajiriwa na Serikali kupitia mpango wa
afya wa Zanzibar kwa lengo la kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa bila ya
usumbufu wowote.
Kwa upande wake Jonathan
Grund Naibu Mkrurugenzi wa mirad Kituo cha Marekani cha Kudhibiti na Kuzuia
Magonjwa amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano katika kuhakikisha kuwa
huduma zinatolewa kwa ufanisi mkubwa na kuipongeza Wizara ya Afya kwa kuchukua
jukumu la kuendeleza huduma hizo hapa nchini
Aidha amefahamisha kuwa CDC itaendelea kuunga mkono jitihada
za Serikali kupitia Wizara ya Afya za kuimarisha mifumo ya utoaji huduma ili
wananchi wa Zanzibar wapate huduma zenye ubora na endelevu.
mwisho
0 Comments