Na Maelezo Zanzibar 17/03/2026
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanza ujenzi na utanuzi wa hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja ili kuimarisha huduma za afya nchini.
Akizungumza katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar wakati akizungumza na waandishi wa habari katika siku 100 za Mafanikio za Uongozi wa Dk. Mwinyi Kaimu Waziri wa Afya Dkt. Saada Mkuya Salum amesema ujenzi huo upo katika hatua za awali ambapo unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba 2027.
Amesema kukamilika kwa ujenzi huo kutasaidia kuimarika kwa huduma za rufaa nchini ambapo hospitali hiyo itatoa huduma ya matibabu ya kibingwa ikiwemo matibabu ya maradhi ya moyo pamoja na kuongeza idadi ya vitanda ili kuongeza ufanisi.
“Ujenzi wa hospitali yetu ya Rufaa ya Mnazi Mmoja unakwenda sambamba na ujenzi wa hospitali ya wazazi ya Mwembeladu ambayo inafanyiwa ukarabati mkubwa katika hospitali hiyo kutawekwa wodi ya watoto wachanga ambao hawajatimia na tayari tumeshaini mkataba na mkandarasi wetu ambae ni China Jiangxi International Economic and Technical Cooporation Company Ltd. JV China IPPR International Engineering Company Ltd” ameeleza.
Aidha Waziri Saada ameeleza kuwa Serikali imepanga kujenga hospitali kila Mkoa ili kuimarisha huduma za afya ambapo ujenzi wa Hospitali hizo umeanza na upo katika hatua mbali mbali ili kuimarisha na kuboresha miundombinu ya afya
Dkt. Saada amefahamisha kuwa Serikali imefanya mageuzi makubwa ya ujenzi wa hospitali za Wilaya na Mkoa ambapo kwa sasa hospital hizo zote zinaendelea kutoa huduma bora za matibabu kwa wananchi pamoja na kuimarisha miundombinu ya Hospitali ya Abdalla Mzee ili iendane na utoaji wa huduma katika viwango vya ngazi ya Hospitali ya Mkoa na Rufaa kwa Pemba tayari imejengewa chumba cha kutoa huduma za uchunguzi kwa kutumia kipimo cha MRI.
Akizungumzia kuhusu ya taifa nguvu kazi ya Taifa Kaimu huyo amafahamisha kuwa imeendelea kuongeza idadi ya wataalamu wa Afya bingwa na bobezi ili kuimarisha usawa katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi kwa kuongeza madaktari bingwa 126 (2024/2025) hadi kufikia 136 (2025/2026) ambapo jumla ya madaktari bingwa 53 wapo masomoni.
“Pia Wizara imeweza kuongeza madaktari bingwa Bobezi kutoka 3 (2024/2025) hadi kufikia daktari bobezi 4 (2025/2026) kwa sasa ikiwemo Daktari bingwa bobezi wa moyo 2, Daktari bingwa bobezi radilogia wanawake,Daktari Bingwa bobezi wa Figo na upandikizaji figo. Aidha, wizara imeongeza wauguzi bingwa kutoka 95 (2024/2025) hadi kufikia 107 (2025/2026) ambapo jumla ya wauguzi bingwa 13 wapo masomoni” ameeleza.
Katika kutekeleza Sera ya Mapinduzi ya utoaji wa matibabu bure kwa wananchi Waziri Saada ameeleza kuwa Serikali itaendelea kutoa huduma hizo kupitia Mfuko maalumu kwa makundi maalum ikiwemo watu wasiojiweza, mama wajawazito, wazee, na Watoto chini ya umri wa miaka mitano ili kufikia lengo la Bima ya Afya kwa Wote ifikapo mwaka 203.
Aidha Waziri Saada amesema kuwa Serikali ianatarajia kuajiri wafanyakazi 1300 katika vituo vya afya na dispensary ili kuimarisha utoajia wa huduma za afya.
Kaimu Waziri wa Afya Dk,Saada Mkuya Salum akifafanua jambo wakati akizungumz a na Waandishi wa Habari kuhusiana na Mafanikio na Maendeleo yaliopatikana katika Wizara kufikia Siku Mia Moja za Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi kwa Kipindi chake cha Pili hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Habari Maelezo Rahaleo Zanzibar.
0 Comments