6/recent/ticker-posts

Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Zanzibar Mhe.Mboja Ramadhan Azungumza na Walimu,Wazazi na Kamati ya Skuli Kujadili Maendeleo ya Skuli ya Matetema

Na Maelezo Zanzibar 12/03/2026

Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda ambae pia ni Naibu Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Mboja Ramadhan Mshenga amewataka wazazi na walimu kuwa kitu kimoja katika malezi ya wanafunzi ili kuleta maendeleo na kuimarika kwa kiwango cha elimu nchini.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na Walimu, Wazazi pamoja na Viongozi wa Kamati ya Skuli ya Msingi ya Matetema, Wilaya ya Kaskazini 'B' Mkoa wa Kaskazini Unguja katika kikao cha pamoja cha kujadili namna bora ya kuwasaidia wanafunzi wa skuli hiyo ili kuweza kufanya vizuri katika masomo yao.

Amesema lengo kubwa la kikao hicho ni kukaa pamoja kujadili namna bora ya kuwasaidia wanafunzi katika kufikia malengo yao katika suala zima la elimu hivyo ipo haja kila mmoja kuchukua nafasi yake ili kuhakikisha wanaongeza ufaulu na kuimarisha elimu Jimboni humo.

Amesema mashirikiano ni kitu muhimu katika kuleta maendeleo  hivyo ni vyyema  kwa walimu na wazazi kushirikiana na kubeba jukumu la kuhakikisha kwamba wanafuatilia nyendo za wanafunzi kuwa wanafika skuli kwa wakati pia wanafanya vizuri katika masomo yao ili kuongeza ufaulu na kufanikiwa kielimu Skuli hiyo.

“Mashirikiano katika malezi ni njia moja ya kuleta maendeleo hivyo ni jukumu la mzazi na walimu kuhakikisha kwamba wanafuatilia watoto wao na kuhakikisha ya wanafunzi wanasoma kwa bidii ili kuongeza ufaulu na kufikia malengo yao ya kielimu  na skuli ya Matetema inasifika kwa kufaulisha vizuri” amefahamisha Mhe. Mboja.

Mwakilishi huyo ameeleza kuwa haridhishwi na matokeo ya mitihani katika Skuli ya Matetema kutokana na wanafunzi wengi kufeli na kurudi nyuma kielimu kwani elimu ndio msingi wa maendeleo na  vijana ndio nguvu kazi ya Taifa hivyo juhudi zinahitajika ili kuimarisha na kukuza kiwango cha elimu na kutengeneza historia mpya ya kupasisha wanafunzi wengi katika Jimbo la Mahonda.

“Sisi viongozi wa Jimbo la Mahonda tupo tayari kuwasililiza na kutoa nguvu zetu, nitafurahi sana kuskia Skuli ya Matetema imefaulisha Wanafunzi wengi na kuacha historia katika Jimbo letu la Mahonda”

Kwa upande wao wazazi, walimu na viongozi wa Kamati ya Skuli ya Msingi ya Matetema wamesema wapo tayari kushirikiana kwa pamoja ili Skuli hiyo iweze kufanya vizuri na kuleta maendeleo kwa jamii na Taifa kwa ujumla.





Post a Comment

0 Comments