6/recent/ticker-posts

POLISI WANAWAKE MOMBA WAMFARIJI BI. JENIPHER KUELEKEA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI


Na Issa Mwadangala.

Katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayoadhimishwa kila mwaka tarehe 08 Machi, 2026, mtandao wa Polisi wanawake TPF-Net Wilaya ya Momba Mkoani Songwe kwa kushirikiana na askari wa kike wa Jeshi la Zimamoto na uokozi Wilaya ya Momba wamemtembelea na kumfariji Bi. Jenipher Kabhole kwa kumpatia msaada wa mahitaji mbalimbali ya msingi.

Tukio hilo limefanyika tarehe 06 Machi 2026 nyumbani kwa Bi. Jenipher Mtaa wa Mtakuja, Kata ya Sogea, Wilaya ya Momba Mkoani Songwe, ikiwa ni sehemu ya kuonesha mshikamano na kuwajali watu wenye uhitaji katika jamii.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Momba, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Fidelia Kasongwa alisema kuwa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani hayalengi kusherehekea pekee, bali pia kutoa faraja na msaada kwa watu wenye mahitaji maalum katika jamii, huku akieleza kuwa ni muhimu taasisi na jamii kwa ujumla kuendelea kuwa karibu na watu wenye uhitaji kwa kuwasaidia mahitaji muhimu pamoja na kuwajali afya zao, ikiwemo kuwapatia bima ya afya ili waweze kupata huduma za matibabu kwa urahisi.

Katika tukio hilo, Bi. Jenipher alikabidhiwa msaada uliokuwa na bima ya afya ya mwaka mmoja, godoro, mafuta ya kupikia lita 5, unga debe 1, gunia la mkaa 1, sabuni miche 2, sukari kilo 2, chumvi kilo 2, blanketi 1, shuka na foronya 2, mchele debe 1 pamoja na kiti cha kukalia na mahitaji mengine ya nyumbani.

 Kwa upande wake, Bi. Jenipher alishukuru kwa msaada huo na kueleza kuwa utasaidia kuboresha maisha yake ya kila siku, huku akiwapongeza Polisi wanawake na askari wa zimamoto kwa moyo wao wa kujitoa katika kusaidia jamii.

Post a Comment

0 Comments