Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Muhamed Mussa amesema Serikali imefanya mageuzi katika sekta ya elimu kwa vitendo ambayo yanaonekana kwa wananchi na kuhakikisha yanaleta taswira mpya ya mwelekeo wa sekta ya elimu nchini.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo, kuhusu siku 100 za mafanikio ya uongozi wa awamu ya pili ya Dkt. Mwinyi amesema mwelekeo sahihi wa Serikali katika kuijenga sekta ya elimu iliyo imara na yenye tija kwa Taifa.
“Tumeshuhudia maendeleo yanayogusa maeneo muhimu ikiwemo ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya elimu, kuendelea kwa utekelezaji wa mitaala iliyoimarishwa, kuimarika kwa matumizi ya Tehama katika kufundishia na kujifunzia, kuimarika kwa ufaulu katika mitihani ya Taifa pamoja na hatua madhubuti za kuendeleza elimu ya juu” ameeleza Waziri Lela.
Amesema kuwa Serikali inaendelea kuweka mkazo katika ujenzi wa madarasa na Skuli mpya kama sehemu ya mkakati wa kuimarisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia ili kutimiza azma ya kuondoa mfumo wa zamu na kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani.
“Kwa kutambua umuhimu wa suala hili, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi imeelekeza ujenzi wa jumla ya madarasa 1,000 kwa ngazi ya elimu ya msingi na madarasa 1,000 kwa elimu ya Sekondari, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Skuli 10 za ghorofa kwa kila ngazi hizo za elimu” amefahamisha Mhe. Lela.
Waziri Lela amefahamisha kuwa, Serikali inaweka mkazo katika kuwajengea vijana ujuzi na stadi za vitendo zitakazowawezesha kujitegemea na kukabiliana vyema na mahitaji ya soko la ajira kwa kuweka mtaala mpya katika ngazi ya elimu ya Sekondari kwenye fani za mafunzo ya amali ili kuwapatia wanafunzi maarifa na ujuzi.
Ameeleza kuwa Serikali katika kuimarisha ubora wa elimu nchini, ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya Taifa kidato cha nne umeimarika ambapo watahiniwa 19,075 wamefaulu sawa na asilimia 91.9 mwaka huu ikilinganishwa na asilimia 82.0 ya mwaka 2024, kiwango hicho cha ufaulu kimezidi shabaha iliyowekwa katika Ilani ya kufikia ufaulu wa asilimia 90 katika mitihani ya Taifa ya kidato cha nne ambapo wanafunzi 150 wamefaulu darajala la I.
“Serikali imeendelea kuimarisha huduma ya utoaji wa mikopo ya elimu ya juu ili kupanua fursa za vijana kupata elimu katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu. jumla ya wanafunzi 8,957 wamenufaika na mikopo ya elimu ya juu, ikilinganishwa na wanafunzi 8,870 waliopatiwa mikopo mwaka 2024. Hatua hii inaonesha mwenendo chanya katika kupanua wigo wa wanufaika,” amefahamisha Mhe Lela.
Amefahamisha kuwa Serikali imepanga kuajiri jumla ya walimu 1,800 ili kukabiliana na uhaba wa walimu katika baadhi ya Skuli pamoja na kupata walimu katika Skuli mpya zinazoendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba.
Amewasisitiza wazazi, walezi na walimu kuwasmamia vyema na kufuatilia kwa karibu nyenendo za wanafunzi ili kuhakikisha wanajikinga na kuepuka vitendo vya udhalilishaji kwa Watoto kwa lengo la kupata mafanikio mazuri katika jamii na kuleta maendeleo imara ya ukuaji wa kiwango cha elimu nchini.









0 Comments