Serikali itaendelea kuzithamini juhudi za wasanii wakongwe kutokana na mchango wao mkubwa kwa kuburudisha kuelimisha pamoja na kukosoa jamii .
Akizungumza katika ziara ya kuwatembelea wasanii wakongwe Waziri wa Habari ,Sanaa, Utamaduni na Michezo Mhe. Dk. Riziki Pembe Juma amesema Serikali itaendelea Kuwaunga mkono na kutafuta njia za kutatua changamoto zao ili kuhakikisha wanaishi katika mazingira bora yenye kustahiki huko Mkoa Mjini Magharibi .
Amesema kuwa ameguswa na hali wanazopitia kwa baadhi ya wasanii wakongwe kwani wao ni sehemu ya historia ya taifa na ndiyo hazina kubwa katika kuelimisha jamii na kuchangia maendeleo ya nchi.
Aidha amesema serikali itaendelea kuweka mikakati madhubuti ili kuhakikisha wasanii wanalipwa stahiki zao kulingana na kazi walizozifanya hatua ambayo inalenga kuimarisha ustawi wa wasanii na kuifanya tasnia ya Sanaa kuwa na thamani zaidi kiuchumi .
Nae Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa, Sensa na Filamu Zanzibar Juma Chum amesema baraza hilo limekuwa na utaratibu wa kuwatembelea na kuwafariji wasanii wakongwe kwa kutambua mchango wao walioutoa kwa kukuza sekta ya sanaa nchini .
Nao Wasanii hao wameishukuru Serikali kwa hatua hiyo ya kuendelea kuwajali na kuwafariji imekuwa faraja kubwa kwao kwani imeonyesha kwamba mchango wao katika kujenga jamii bado unatambuliwa na kuthaminiwa .
Wasanii hao wamesema kuwa kazi zao za Sanaa hazikuwa rahisi kwani zilihitaji kujitolea na kujituma kwa muda mrefu ili kuhakikisha Sanaa inatumika kama chombo cha kuelimisha na kuhamasisha jamii .
Aidha wasanii hao wameeleza kwamba kupitia nyimbo na maigizo waliweza kufikisha ujumbe muhimu uliosaidia kujenga maadili na kuhamasisha maendeleo ya jamii .
Katika ziara hiyo imejumuisha Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo pamoja na Viongozi na wafanyakazi wa baraza la Sanaa,Sense na Filamu Zanzibar waliwatembelea wasanii wakongwe akiwemo Mzee Chimbeni Kheir pamoja na Mzee Khamis Mussa Akida .
hatua ya kuwatembelea wasanii wakongwe inaonyesha umuhimu wa kuthamini mchango wao walioutoa kupitia sanaa zao ikiwa ni juhudi ya kuhifadhi historia na urithi wa utamaduni wa Zanzibar kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
imetolewa na Kitengo cha Habari .
WHSUM.






0 Comments