Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amewakumbusha wazazi na walezi kuwasimamia watoto wao katika kupata elimu ya Dunia na Akhera zitakazowajenga kuwa watoto wema na kupelekea kuwa na Taifa lililo bora.
Alhajj Hemed ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameyasema hayo wakati akikabidhi MADRASATU HIDAYA na MADRASATU SWABIRINA alizozijenga katika Jimbo la Kiwani ikiwa ni miongoni mwa kutimiza ahadi zake alizoziweka wakati akiomba ridha ya kuwa mwakilishi wa Jimbo hilo.
Amesema lengo la kujenga Madrasa hizo ni kuwawekea mazingira mazuri wanafunzi ili wawe na sehemu salama ya kukisoma kitabu kitakatifu cha Qur'an hatua ambayo itapelekea kupata jamii bora na yenye maadili mema.
Alhajj Hemed ameeleza kuwa dhamira ya viongozi wa jimbo la Kiwani ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wa Madrasa zote wanakuwa mstari wa mbele katika kuifahamu Qur'an ipasavyo, kuihifadhi na kukifanyia kazi katika maisha yao ya Kila siku.
Aidha, amewasisitiza mwananchi kuhakikisha wanawasimamia vijana wao katika suala zima la kuhifadhi Qur-ani ili kuweza kupata vijana watakaoliwakilisha Jimbo la akiwani katika mashindano makubwa ya Qur-an kwenye nchi mbali mbali duniani.
Sambamba na hayo Alhajj Hemed amewataka wazazi na walezi kushirikiana na walimu katika kuitunza miundombinu ya madrasa ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuwanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.
Alhajj Hemed amesema endapo wazazi watawalea watoto wao katika misingi iliyoelekezwa katika Qur'an kutasaidia kupunguza matendo maovu katika jamii ikiwemo ubakaji, udhalilishaji, wizi na uporaji.
Akizungumzia Miradi mengine ya Maendeleo katika Jimbo la Kiwani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewahakikishia Wananchi wa Jimbo hilo kuwa Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi itajenga Barabara inayoelekea Michakweni kwa kiwango Cha Lami muda mchache ujayo.
Ameeleza kuwa Serikali imetenga zaidi ya Bilioni mbili za Kitanzania kwa ujenzi wa Diko ambapo tayari Serikali imeshazungumza na Mkandarasi na kumuelekeza kuwa kazi zote za usaidizi wa ujenzi wapatiwe wannachi wazawa.
Wakitoa shukurani kwa kukamilika ujenzi wa madrasa hizo, wananchi wa Kiwani wamemuhukakikishia Mwakilishi huyo kuwa watahakikisha wanawasimamia vyema watoto wao katika kupata elimu bora yenye kuwakuza katika maadili mrma na kuwajenga kuishi maisha yenye kumpendeza mwenyezi Mungu.
Akisoma Taarifa ya Kitaalam Mkandarasi wazawa kutoka kampuni ya FAHARI CONSTRUCTION Bwana MOH'D ABDALLAH RASHID ameeleza kuwa Ujenzi wa Madrasa hizo unajumuisha Madrasa ya kusomea, Ofisi za Walimu pamoja na vyoo ambapo miundombinu yote stahiki ikiwemo Umeme, Maji na Samani vimeweka ndani ya madrasa hizo.
Mhandisi MOH'D amesema ujenzi wa madrasat Hidaya umegharimu Shilingi 36,737,400/= (Millioni Thalathini na Sita, Laki Saba na Thalathini na Saba na Mia Nne) ambapo Shilingi 67,150,000/= (Millioni Sitini na Saba, Laki Moja na Khamsini Elfu) zimetumika katika ujenzi wa Madrasatu Swabirina ya Kiwani
Nae Mratibu Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar Pemba Shekh Said Ahmad ameeleza kuwa Ujenzi wa Madrasa hizo utarahisisha upatikanaji wa Elimu ya Dini kwa watoto na watu wazima wa eneo hilo.
Sheikh Said amemshukuru Mhe. Hemed kwa kuona umuhimu wa kujenga Madrasa hizo ikiwa ni katika juhudi zake za kukuza Malezi mema Jimboni humo.
Imetolewa na Kitengo cha Habari ( OMPR )
Leo tarehe …04 / 03 / 2026



0 Comments