Habari za Punde

KIKAO - KERO ZA MUUNGANO KUJADILI MAFUTA

Ni mapendekezo Wawakilishi kutaka yawe ya Zanzibar


Na Mwantanga Ame -Zanzibar leo ya tarehe 18-5-2009


MAPENDEKEZO ya Wananchi wa Zanzibar, kuhusu suala la Mafuta na gesi asilia kutolewa katika mambo ya Muungano kesho yatawasilishwa katika kikao cha kutatua kero za Muungano.


Hatua hiyo ni baada ya Wananchi wa Zanzibar kupitia Baraza la Wawakilishi Zanzibar katika kikao cha Mkutano wa 14 Aprili mwaka huu kuamua kwamba suala hilo lisiwe la Muungano.


Wajumbe wa Majimbo yote ya Unguja na Pemba, Watendaji Wakuu wa serikali na Wajumbe wa viti vya Kuteuliwa kwa nafasi za Wanawake walipiga kura ya maoni iliyosimamiwa na Spika wa Baraza hilo Pandu Ameir Kificho.


Wajumbe walitaka suala la usimamizi udihibiti na uendeshaji wa shughuli zote za uchimbaji na utafiti wa nishati ya mafuta kusimamiwa na serikali ya Zanzibar.


Pendekezo jengine lililotolewa na wajumbe hao ni Zanzibar kuunda chombo kitakachukuwa na kazi ya kusimamia shughuli za mafuta na gesi itakayopatikana Ukanda maalum wa Uchumi (EEZ).


Pia Wajumbe hao walikataa pendekezo la tatu la serikali iliyotaka ukanda wa Bahari Kuu nao uendeshwe kwa pamoja na kupendekeza litolewe katika mambo ya Muungano.


Baada ya mapendekezo hayo Waziri Kiongozi wa Serikali ya Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha, aliwaahidi Wajumbe wa Baraza hilo alipohotubia kufunga kikao hicho kwamba atayawasilisha katika kikao cha kujadili kero za Muungano kitachofanyika kesho.


"Nikiwa Msimamizi Mkuu wa shughuli za serikali, nitasimamia vyema suala hili, tumeyapokea maamuzi mlioyafanya na tutayafanyia kazi kadri mlivyoshauri waheshimiwa Wawakilishi", alisema Nahodha.



Akizungumza na Zanzibar Leo, Waziri wa Nchi Afisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma, alisema ni kweli kikao hicho kitafanyika kesho Mjini Dar es Salaam.


Alisema kabla ya kuanza kikao hicho, leo kitafuatiwa na kikao kitakachowashirikisha Mawaziri wa Wizara ambazo zinahusiana na kero za Muungano zilizopo sasa katika Mkataba wa Muungano wa Tanzania.



Alisema kikao hicho ni kwa ajili ya kupitia taarifa zilizotolewa katika kikao kilichofanyika Hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar, huku wakiangalia maagizo yaliotolewa jinsi yalivyoweza kufanyiwa kazi.



Waziri huyo alisema suala la mafuta na gesi asilia litafikishwa katika kikao hicho kwa vile ajenda yake ilikuwa ni miongoni mwa zilizotolewa katiks kikao kilichopita na kutaka kuachwa ifanyiwe kazi kwa kumpa muda mtafiti aliyepewa kazi hiyo David Reading amalize kazi yake.


Alisema kwa vile serikali zote mbili tayari zimekabidhiwa ripoti hiyo na kutoa mapendekezo yake katika kikao hicho ajenda hiyo itaweza kujadiliwa.Alifahamisha kuwa kikao hicho kitafanyika kesho ambapo kitasimamiwa na Waziri Kiongozi wa Zanzibar Shamsi Vuai Nahodha na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Dk. Ali Mohammed Shein.


Mijadala mengine inayotarajiwa katika kikao hicho ni pamoja na suala la kero za Wafanyabiashara kutozwa kodi mara mbili pale wanaposafirisha bidhaa zao kutoka Zanzibar kwenda Tanzania bara.



Hicho kitakua ni kikao cha pili cha kutatua kero za Muungano kukaa kwa mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.