Habari za Punde

OCEAN VIEW YASHINDA KWA TAABU

Na Ameir Khalid

TIMU ya Zanzibar Ocean View, imeanza vyema kampeni za kutetea ubingwa wake kwa kuwalaza wanagenzi wa ligi hiyo timu ya Chuoni bao 1 -0 kwenye uwanja wa Mao Tsetung juzi.

Hata hivyo ushindi huo haukupatikana kirahisi, kwani maustaadh wa Chuoni walionesha soka la ushindani na hadi timu zinakwenda kupumzika, hakuna nyavu iliyokuwa imehujumiwa.

Katika kipindi cha pili, wanaume hao waliendelea kukamatana sawasawa hadi mnamo dakika ya 79 pale Ocean View ilipofanya shambulio la nguvu langoni mwa Chuoni.

Wakati mchezaji Mohammed Abdulrahman akielekea kumuona mlinda mlango wa Chuoni aliangushwa ndani ya sanduku na muamuzi Waziri Sheha hakusita kuamuru mpira wa penelti.

Mkwaju wa penelti uliopigwa na Hassan Seif Banda ulipanguliwa na golkipa wa Chuoni na kurudi uwanjani kabla Banda kuusukumiza tena nyavuni, na kuzua malalamiko kutoka kwa wachezaji na viongozi wa Chuoni waliodai kuwa mfungaji aliotea.

Mchezo huo ulilazimika kusimama kwa dakika kadhaa baada ya wachezaji kurushiana ngumi, kabla muamuzi kuwaonesha kadi nyekundu Suleiman Mussa na Makame Haji wa Chuoni, pamoja na Aziz Shaweji na Farouk Ramadhani wa Zanzibar Ocean View.

NAYE MASANJA MABULA anaripoti kutoka Pemba kuwa maafande wa Duma walilazimishwa sare ya magoli 2-2 na wanagenzi wengine wa ligi hiyo Madungu United katika uwanja wa Kinyasini Wete.

Magoli ya Duma katika pambano hilo lililokuwa la kuvutia, yalinasishwa nyavuni na Salim Nassor na Ame Ali, huku Rashid Othman akiifungia Madungu mabao yote mawili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.