Na Salum Vuai, Maelezo
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ramadhan Abdallah Shaaban, asubuhi hii anatarajiwa kubariki sherehe za maadhimisho ya siku ya Kiswahili Zanzibar.
Maadhimisho hayo yamepangwa kufanyika katika ukumbi wa EACROTANAL kuanzia saa tatu asubuhi ambapo wadau wa lugha ya Kiswahili, wataalamu na wasomi mbalimbali wamealikwa kuhudhuria.
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA), Khadija Bakari Juma, maadhimisho hayo mwaka huu, yatajumuisha mada tatu zitakazowasilishwa ikiwemo 'Maadili yetu ni kinga dhidi ya ukimwi'.
Mada nyengine alisema, ni 'Athari ya mimba za utotoni' pamoja na 'Kazi za amali'.
Aidha alifahamisha kuwa sherehe hizo zitaambatana na utoaji zawadi kwa washindi wa tenzi walioshiriki shindano lililoandaliwa na Baraza hilo, katika mikakati yake ya kukikuza Kiswahili na kuhamasisha matumizi sahihi ya lugha hiyo.
Katibu Mtendaji huyo alifahamisha kuwa kutakuwa na uzinduzi wa kitabu kipya kilichoandikwa na BAKIZA, kiitwacho 'Makala za semina ya kumuenzi mwandishi Mohammed Said Abdullah (Bwana Msa)'.
Alisema kuwa kitabu hicho kimetungwa kutokana na makala mbalimbali zilizowasilishwa katika semina ya kumuenzi mwandishi huyo mashuhuri na mahiri wa riwaya Afrika Mashariki, iliyofanyika mwaka 2007.
Tukio jengine litakalopamba hafla hiyo, alisema ni kusoma kumbukumbu za baadhi ya wasanii na wanafasihi wa Zanzibar waliotangulia mbele ya haki, ambapo mara hii wamechaguliwa watano ambao ni Seif Salim Saleh (Ikhwan Safaa), maalim Ameir Issa, maalim Haji Chum, Ali Omar Baramia pamoja na Mohammed Said Abdullah (Bwana Msa).
Fikra ya kuanzisha siku maalumu ya Kiswahli Zanzibar, ni mawazo yaliyoibuka wakati wa semia ya kumuenzi Bwana Msa mwaka 2007.
Miongoni mwa watu mashuhuri walioalikwa katika tukio hilo ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdallah Mwinyi Khamis, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Abdilahi Jihad Hassan na wadau mbalimbali wa lugha hapa nchini.
No comments:
Post a Comment